Miongoni mwa Mechi hizo 8, City, walio
chini ya Meneja Manuel Pellegrini, imeshusha vipigo kwa Mabingwa
Watetezi Man United Bao 4-1, Tottenham 5-0 na Arsenal 6-3.
Lakini, safari hii, wageni wa City ni
Liverpool ambao wanaongoza Ligi katika Kipindi hiki cha Krismasi kwa
mara ya kwanza tangu Msimu wa 2008/09 na wanae Straika bora kwa sasa
Luis Suarez ambae ndie Mfungaji Bora akiwa na Bao 19.
JE WAJUA?
-Liverpool wameshindwa kuwa Bingwa katika mara zote tatu za mwisho walizoongoza Ligi wakati wa Krismasi.
-Mara hizo 3 ni 1990-91
walipomaliza Nafasi ya 2, Mwaka 1996-97 walipomaliza Nafasi ya 4 na
2008/09 walipomaliza Nafasi ya 2 nyuma ya Man United.
Hata hivyo, Liverpool wakiwa Ugenini ni nyanya kidogo na katika Mechi zao 8 za Ligi za Ugenini wamefungwa Bao 13
Wachambuzi wengi walikuwa na hamu na
Mechi hii kuwaona Mastraika wanaong’ara Sergio Arguero wa City na Luis
Suarez wakipambana uso kwa uso lakini, kwa bahati mbaya, Aguero
hatakuwepo kwa vile ni Majeruhi na badala yake City wanaweza kumchezesha
Alvaro Negredo au Edin Dzeko.
-Mechi 6 kati ya 9
zilizopita za Ligi kati ya City na Liverpool zilimalizika kwa Sare huku
City wakishinda 2 na Liverpool 1 Uwanjani kwao Anfield kwa Bao 3-0.
Lakini nguzo kubwa ya Timu ya City ni
Kiungo chao hatari ambacho Msimu huu kimeimarika baada kumpata
Fernandinho ambae ameonyesha ushirikiano mzuri sana na Yaya Toure kiasi
cha kuwaruhusu David Silva na Jesus Navas kuwa huru kutiririka na Soka
lao lenye akili ambalo huzichanganya ngome nyingi na kutoa mwanya wa
Goli nyingi.
Kwa kawaida kukosekana kwa Mkongwe na
Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard, kungekuwa pigo kubwa kwa Liverpool
lakini katika Mechi za hivi karibuni kutokuwepo kwake kwa sababu ya
maumivu kumefungua njia kwa Liverpool kutumia Viungo Chipukizi, kina
Allen, Lucas, Henderson, Coutinho na Sterling, wanaokwenda mbio
mithili ya umeme na kumlainishia umaliziaji Luis Suarez.