Kocha mpya wa Azam fc Joseph Marius Omog hana wasiwasi na wapinzani wao Ferreviario De Beira
![]() |
Benchi la ufundi la Azam kushoto ni Kalimangonga Ongala na Joseph Omog |
Ratiba
ya michezo ya vilabu barani Afrika hususani kombe la shirikisho
iliyotolewa jana na shirikisho la soka barani Afrika CAF ni wazi kabisa
kuwa haimnyimi usingizi kocha mpya wa Azam fc ya Tanzania Mcameroon
Joseph Marius Omog ambaye amechukua mikoba ya mwingereza Stewart John
Hall kwa mkataba wa miaka miwili.
Kwa
mujibu wa ratiba ya CAF ya michuano ya kombe la shirikisho ni kwamba
Azam fc itaanzia ugenini dhidi ya Ferreviario De Beira ya Mozambique
mchezo ambao bila shaka utafanyika huko Beira.
Hii
ni ratiba nyepesi ya kuanzia kwa upande wa Azam fc ambao huu kwao ni
msimu wa pili mfululizo wanashiriki michuano hii ya vilabu barani
Afrika.
Itakumbukwa
msimu wa mwaka 2012/2013 Azam ambayo ilikuwa ikiingia kwenye uzoefu
mpya wa michuano ya vilabu barani Afrika waliaanza na Al Nasri Juba ya
Sudan Kusini jijini Dar es Salaam ilikuwa ni tarehe 16/02/2013 na Azam
waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 huku mabao hayo yakifungwa na Abdi
Kassim 'Babi' na Kipre Tchetche kabla ya kuikandamiza tena katika uwanja
wa ugenini katika mchezo wa marudiano kwa mabao 5-0 yaliyofungwa na
Hamisi Mcha Vialli mabao 3 Hat-trick , John Boko na Salum Abubakar
'sureboy'.
Azam ilipita na kutinga roundi ya pili kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1.
Umony wa Azam akimpongeza Babi kwa kumshika kichwa baada ya kufunga goli dhidi ya Al Nasri Juba |
Katika
raundi ya pili Azam fc ilikutana dhidi ya Barrack Y.C 11 ya Liberia
ambapo mchezo wa kwanza ilichezwa tarehe 17/03/2013 nchini Liberia
ambapo Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na Humphrey
Mieno na Seif Abdalah 'Karihe' kabla ya mchezo wa marudiano uliopigwa
uwanja wa taifa jijini Dar es Salam tarehe 05/04/2013 ambao ulimazika
kwa suluhu 0-0, ambayo iliiwezesha Azam fc kutinga hatua iliyofuata ya
ikipangiwa kucheza dhidi ya Waarabu wa FAR Rabat ya Morocco, ambapo
walikwenda suluhu 0-0 mchezo wa kwanza uwanja wa Taifa kabla ya kupokea
kichapo cha bao 2-1 ugenini Rabat na kumaliza safari yao ya michuano
hiyo.
Kwanini
nilianza kwa kusema ratiba iliyotoka hamnyimi usingizi, ni kwasababu
kocha huyu mwenye umri wa miaka 42 ana uzoefu mkubwa na mashindano ya
vilabu Afrika, achilia mbali kuifundisha timu ya taifa ya Cameroon ya
wachezaji wa ndani CHAN 'Indomitable
Lions' lakini pia kwa upande wa vilabu alifanya vema akiwa na AC
Leopards ambao ni vigogo wa soka nchini Congo Brazaville.
Imani
kubwa hapa ni kwakuwa Azam fc tayari imesha pata uzoefu kwenye michuano
ya vilabu Afrika na ilipoishia msimu uliopita si haba, lakini pia kwa
kuwa na kocha mwenye uzoefu mkubwa wa kiwango hiki katika klabu hii
ambayo imekuwa na miundo mbinu yakinifu ya kisoka yenye mwelekeo wa
kubadili utamaduni hasi uliozoeleka wa soka la Tanzania lisilo kuwa la
uwekezaji, isipokuwa porojo na fitna, basi huenda wakadhihirisha hilo
katika michuano ijayo ya vilabu Afrika wakiwakilisha kwa mara ya pili
katika michuano ya kombe la shirikisho.
Mafanikio ya Joseph Marius Omog kuiwezesha AC
Leopards ya Congo Brazaville kutwaa mara mbili taji la ligi ya soka ya
nchi hiyo na kuweka histori kubwa barani Afrika kwa mara ya kwanza
katika kipindi cha miaka 38 kupeleka taji la michuano ya kombe la
Shirikisho nchini Congo, hiyo yatosha Azam fc Kujivunia kuwa na kocha
mwenye kaliba kama hiyo klabuni hapo kama kocha mkuu.
AC
Leopards iliichapa Djoiba ya Mali ushindi wa jumla wa mabao 4-3
uliotokana na sare ya mabao 2-2 ugenini mjini Bamako kabla ya kuwafunga
2-1 mjini Brazaville.
Sifa
kubwa ya makocha ni kutwaa makombe kama ilivyo kwa Omog ambaye tayari
ameshavaa zawadi kubwa ya ubingwa barani Afrika na hivyo kumfanya kunywa
maji ya baridi yenye barafu huku akisikilizia raha ya ubaridi wake
kooni kwani ratiba yake ya mchezo wa kwanza ni nyepesi.
Ni
wazi kuwa katika michuano iliyopita ya vilabu Afrika timu kutoka
Mozambique Liga Muculmana iliwafungisha virago Gaboroni United ya
Botswana kwa ushindi wa mabao 3-2 katika hatua ya awali ilhali timu ya
Gaboroni United ni moja kati ya timu nzuri ukanda wa kusini mwa Afrika.
Baadaye
tena katika raundi ya pili Muculumana iliwafungisha virago Lobi Stars
ya Nigeria kwa mabao mengi ya ushindi wa jumla wa 8-4 baada ya ushindi
wa kushangaza wa mabao 7-1 katika mchezo wa pili wa marudiano.
Ni wazi kuwa soka la msumbiji kwa kiwango cha vilabu si baya sana lakini uzoefu wa kocha Joseph Marius Omog
ni chachu ya kuiwezesha Azam fc kuwadhoofisha wapinzani wao
Ferreviario de Beira ya Mozambique katika mchezo wa raundi ya kwanza ya
kombe la shirikisho barani Africa.