Golikipa bora wa michuano ya Mapinduzi, 2015… SAID MOHAMMED- Mtibwa Sugar
Hata kabla hajacheza mkwaju wa
penalti wa kiungo Shaaban Kisiga, tayari golikipa wa Mtibwa Sugar, Said
Mohammed alionesha kiwango kikubwa katika michezo mitano ya mwisho.
Akiwa ameruhusu bao moja tu (sawa na Manyika Peter wa Simba SC), Said
alikuwa bora katika uchezaji wa mipira ya krosi na mashambulizi ya moja
kwa moja.
Aliibeba timu yake dhidi ya Azam
FC katika robo fainali baada ya kucheza mikwaju ya penalti, pia
aliisaidia sana timu yake katika nusu fainali dhidi ya Polisi na
alikaribia kuwapa taji katika mchezo wa fainali kama si Ibrahim Jeba
asingepoteza mkwaju wa penalti wakati Mtibwa wakiwa mbele. Said
alistahili hakika kuwa golikipa bora wa michuano…
02; HASSAN KESSY-Simba SC Alitajwa kama mchezaji bora wa mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi wakati Simba ilipoicharaza, Taifa ya Jang’ombe kwa mabao 4-0, Kessy amekuwa namba mbili bora katika timu yake licha ya kuichezea michezo tisa tu ta ngu asajiliwe akitokea Mtibwa mwezi Disemba. Aliipandisha timu kwa kasi, alionekana mwenye nguvu kila alipogombania mpira, alipendeza namna alivyomkaba mshambulizi Musa Hassan Mgosi katika michezo miwili waliyokutana katika siku 13 za michuano hiyo.
Katika mchezo wa fainali, Kessy
alimzima kabisa Mgosi hadi kupelekea mshambulizi kuoneshwa kadi ya
njano. Kwa miaka miwili sasa, Kessy anathibitisha mtazamo wa walio wengi
kuwa ndiye mlinzi bora wa kulia kwa sasa nchini. Wakati Shomari Kapombe
ameonekana ‘ ku-hodhi’ nafasi ya ‘ beki 2′ katika timu ya Taifa, Taifa
Stars mlinzi huyo wa klabu bingwa Bara anatakiwa kuwa makini zaidi na
kuzidi kujiimarisha kwani nafasi hiyo iko mbioni kupata ‘ mtu mpya’,
wenyewe wanamuita ‘ Dan Alves’ namaanisha Hassan Kessy Ramadhani.
03: MOHAMMED HUSSEIN ‘ TSHABALALA’.- Simba SC
Hili jina la Tshabalala
limetokea wapi?. Labda maskani za vijana wa kihuni maeneo ya Magomeni
katikati ya jiji la Dar es Salaam, huko unaweza kupata majibu, lakini
kwangu linapotamkwa jina hilo namkumbuka mfungaji wa bao la kwanza la
fainali za kombe la dunia ‘ WOZA2010′ nchini Afrika Kusini. Huyu alikuwa
kiungo mshambulizi akitokea katikati ya uwanja huku akitumia zaidi mguu
wa kushoto.

Moja kati ya matukio ya kukumbwa
sana katika fainali hizo zilizofana ni bao la Siphiwe Tshabalala dhidi
ya Mexico ambalo lilikuwa goli la kuongoza katika mchezo wa ufunguzi
ndani ya uwanja wa Soccer City, baada ya mchezo huo jina la Tshabalala
likawa juu, huku likitamkwa mara kwa mara na mashabiki wa kandanda
barani Afrika. Tumeona mengi kutoka kwa Tshabalala halisi, lakini
najiuliza huyo ‘ Tshabalala wa Simba’ amepataje jina hilo. Achana na
kuboronga kwa timu hiyo katika ligi kuu, ukirudi katika uhalisia
utaungana nami naposema Mohammed Hussein ‘ Tshabalala’ ndiye mchezaji
bora wa Simba katika michezo 14 ya ki-mashindano tangu kuanza kwa msimu
wa 2014/15.
Anavutia anavyozuia, utapenda
kumuona anaposhambulia. Katika mchezo wa fainali aliweza kumdhibiti
vilivyo kijana hatari wa ‘ rika lake’, Ally Shomari ambaye amekuwa
mchezaji wa hatari katika safu ya mashambulizi ya Mtibwa. Kabla ya
michuano hiyo na hata baada ya kucheza michezo miwili ya mwanzo dhidi ya
Mtibwa na Mafunzo safu ya ulinzi ya Simba ilionekana ‘ kucheza kwa
ku-yumba, yumba’.
Hilo lilichangiwa na namna safu
za pembeni katika ‘ fullbacks’ kufanya makosa yasiyo ya lazima. Sasa
Simba wamekuwa salama katika michezo mitano mfululizo ambayo wamecheza
bila kuruhusu bao, yote imechangiwa na vijana, Kessy katika ‘ beki 2′ na
Tshabalala katika ‘ beki 3′. Wanashambulia kwa zamu, mmoja anakwenda,
mwingine anabaki kusubiri kucheza ‘ coverage’ inapotekea wameshambuliwa
kwa shambulizi la kushtukiza ‘ counter attack’.
04; HASSAN ISIHAKA ‘ Captain mtoto’- Simba SC
Unapokosa timu imara za Taifa
katika ngazi ya chini si rahisi kupata mafanikio katika ngazi ya juu kwa
kuwa unakwenda kushindana na timu zenye wachezaji waliokomaa
kiushindani zaidi yako na wenye uzoefu. Laiti vijana kama, Kessy,
Tshabalala, Isihaka wangeendelea kucheza mfululuzo katika michuano ya
kimataifa ngazi ya vijana ingewasaidia sana kuwajenga kuelekea timu ya
Taifa Stars.
Lakini wataendelea kudumaa katika
soka la ndani licha ya kuonesha ukomavu na viwango vya juu katika klabu
yao kiasi cha kuaminiwa katika kikosi cha kwanza. Bila shaka umemuona
Isihaka, beki wa kati-mtulivu, aliyejipanga na kuwaongoza wenzake muda
wote wa michuano. Nyota njema huoneka asubuhi, kijana Isihaka amefuata
nyanyo za Shomari Kapombe naye amekuwa ‘ kiongozi, nahodha kijana’
kuiongoza Simba kutwaa taji. Ndiye beki nne bora katika kikosi changu
cha michuano.
05; SALIM MBONDE- Mtibwa Sugar
Mtibwa ilimsajilili mlinzi huyo
wa kati kutoka timu ya U20 ya JKT Oljoro katikati ya mwaka 2012 na
hakuna shaka tena kuwa uamuzi huo uliofanywa na kocha Mecky Mexime
umekuwa na ‘ bahati kubwa’ katika soka la Tanzania. Mbonde anawakumbusha
watu namna Tanzania ilivyo na vipaji vikubwa. Mtu makini, mtulivu,
mwenye busara na mgumu kupitika. Alitajwa kama mchezaji bora wa michuano
licha ya timu yake kupoteza mchezo wa fainali.

Alijiamini muda wote alipokuwa na
mpira, huku akiwaongoza vijana wenza Ally Lundenga, Vicent Andrew na
mzoefu, David Luhende kucheza mchezo wa kutotanuka hata pale Simba
waliposhambulia kwa nguvu. Sasa Tanzania inacheka, furaha na kicheko
hicho kinaletwa na vipaji timilifu kama cha Mbonde. Kama ukiambiwa
uchague wachezaji bora wa safu ya kati katika ngome bila shaka hata
ukiwa usingizi utawataja, Isihaka na Mbonde, vijana makini na watulivu.
Wakati wa usajili wa mwezi Agosti
kiongozi mmoja wa Simba alimfuata Mbonde na kumwambia ‘ tunataka
kukusajili wewe ni sehemu ya mipango yetu’. Mbonde hakupingana naye
zaidi akamwambia kiongozi huy wa ‘ mnyama’ aende akazungumze na klabu
yake kwa kuwa bado ana mkataba wa miaka miwili. Kila kitu kilikwama
baada ya kiongozi huyo kumwambia mchezaji akavunje mkataba wake na
Mtibwa wao wataingia kumalizia mchakato wa usajili jambo ambalo Mbonde
alilikataa na kulifikisha kwa uongozi wake. Wangejua…, itapendeza siku
Isihaka akihamia Mtibwa ili akacheze na Salim, au Mbonde kuhamia Simba
siku akacheze na Isihaka katika ngome ya kati.
06; JONAS MKUDE.-Simba SC
Katika nafasi hii kuna wachezaji
kadhaa wamefanya vizuri, Mudathir Yahya wa klabu ya Azam FC, Salum
Telela wa Yanga SC lakini nilihitaji mchezaji bora zaidi na bila
wasiwasi nitampanga Mkude, kiungo wa ulinzi wa Simba SC ambaye alicheza
kwa kiwango kilekile tu. Nahodha wa Mtibwa, Shaaban Nditti alicheza kwa
kiwango cha juu katika mchezo wa fainali, hata Henry Joseph pia ameweza
kucheza vizuri . Mkude anapanga mshambulizi vizuri, anashambulia na
kuzuia kwa wakati husika hana cha kutuonesha zaidi ya kuendelea
kujitunza kwa kuwa hana mpinzani katika nafasi hiyo, huyu pia ni kijana
aliye chini ya U21.
07; SAIMON MSUVA.-Yanga SC
Wala huitaji kuumiza kichwa ili
kumpata mchezaji wa nafasi hii, unapoona kiungo wa kulia akifunga mabao
manne katika michezo minne bila shaka unashawikika kuamini ni mchezaji
bora. Licha ya Yanga kuondolewa katika robo fainali, Msuva amefanikiwa
kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa michuano. Uchezaji wake wa kasi, ujanja
na mbinu za kufunga mabao yasiyotarajiwa vinamfanya nimuweke katika
kikosi change bora cha michuano. Ni winga wa kizamini ambaye anaweza
kucheza katika mfumo wowote wa kisasa na kutoa matunda.
08; MUDHAMIR YASINN- Mtibwa Sugar
Alicheza kwa kiwango cha juu
dhidi ya Azam FC katika robo fainali, akafanya hivyo tena katika mchezo
wa nusu fainali dhidi ya JKU, na namna alivyocheza dhidi ya Simba SC
katika mchezo wa fainali nimeshawika kumpanga mchezaji huyo chipukizi
katika nafasi ya kiungo wa mashambulizi. Licha ya Mtibwa kufunga mabao
matatu tu katika michezo sita ya michuano hiyo, Yassin aliweza kuifanya
timu hiyo kuwa ngumu kupitika katikati ya uwanja.
Akishirikiana na Nditti na Mussa
Nampaka mchezaji huyo ameonekana kucheza kwa kujiamini mno huku akipanga
mashambulizi na kupiga pasi za uhakika kwa washambuliaji wake.
Alikimbia pale timu ilipokuwa katika spidi, na alipoa huku akitafakari
namna ya kupora mipira. Akicheza na Mkude katikati ya uwanja itakuwa ‘
balaa’.
09; KPAH SHERMAN-Yanga SC
Ni mshambulizi pekee wa kati
aliyeonesha kiwango kizuri katika michuano hiyo. Mliberia huyo anaingia
katika kikosi change bora ikiwa amefunga mabao mawili katika michezo
minne aliyocheza. Alionesha mwenye uwezo wa kumiliki mpira, kujipanga na
umaliaji wa kiwango cha mchezaji wa kimataifa. Anaingia katika kikosi
hiki kama mshambulizi wa kwanza.
10; DANNY SSERUNKUMA-Simba SC
Ni wachezaji wawili tu wa kigeni
ambao wamepata nafasi katika kikosi hiki, baada ya Sherman wa Yanga SC,
Mganda, Danny Sserunkuma pia anaingia kama mshambulizi wa pili. Danny
hajafunga bao katika michuano hiyo lakini namna alivyokuwa akijipanga,
kutoa pasi, kumiliki mpira na utoaji wa pasi kwa wenzake ndiko
kumechangia kwa kiasi kikubwa safu ya mashambulizi ya Simba kuwa na
kasi. Ni mshambuaji bora wa pili katika michuano ambaye alimiza majukumu
yake vizuri, ndiye aliyepiga penalti ya mwisho ya Simba kabla ya
golikipa Ivo Mapunda kucheza mkwaju wa Vicent Barnabas na kuipa taji
timu yake.
11; RAMADHANI SINGANO-Simba SC
Singano alikwenda Zanzibar
akishutumiwa kushuka kwa kiwango chake, lakini michuano ya Mapinduzi
imeweza kuwaonesha watu namna mcheaji huyo wa kiungo akitokea pembeni ya
uwanja alivyo mkali. Alikuwa na kasi, ufundi huku bao lake la mkwaju
uliokufa dhidi ya JKU katika mchezo wa nusu fainali likibaki kuwa
miongoni mwa mabao bora zaidi katika michuano. Alikuwa mkali na
alifanikiwa kufunga mabao mawili. Andrey Coutinho wa Yanga pia alifanya
vizuri katika michuano hiyo ikiwemo kufunga mabao matatu katika michezo
minne ila nampanga Singano katika nafasi hii kwa kuwa ametuonesha kuwa
tulikosea kumsema, ameanza kuchuja.
