Social Icons

Pages

Sunday, 8 February 2015

WAJUA HISTORIA YA AFCON .MPAKA JANA BINGWA APATIKANE HII HAPA...TWENDE SAWA

KOMBE la Mataifa ya Afrika (CAN),
ndiyo michuano mikubwa ya soka
katika bara la Afrika inayoandaliwa na
Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kwa mara ya kwanza, michuano hii
ilifanyika mwaka 1957 na kuanzia
mwaka 1968 ndipo utaratibu wa
kuchezwa kila baada ya miaka miwili
ulipoanza.

Katika mashindano ya kwanza mwaka
1957 timu shiriki zilikuwa kutoka
mataifa matatu tu yaani, Misri, Sudan
na Ethiopia.

Nchi nyingine ambayo ilitajwa
kushiriki katika mashindano haya ni
Afrika Kusini ambayo hata hivyo
ilinyimwa nafasi hiyo kutokana na
sera zake za ubaguzi wa rangi kwa
wakati huo.

Baada ya hapo mashindano
yameendelea kukua na kuzihusisha
nchi nyingi zaidi na hivyo kuwezesha
kuwapo kwa utaratibu wa mashindano
ya awali ya kusaka tiketi ya kushiriki
fainali zenyewe na hatimaye timu
shiriki kufikia 16.

Historia ya Kombe la Mataifa ya Afrika
inaanzia Juni mwaka 1956 katika
mkutano wa tatu wa FIFA mjini Lisbon,
Ureno, baada ya kiubuka wazo la
kuanzishwa kwa CAF.

Hapo jambo kubwa lililofikiriwa ni
kuanzishwa kwa mashindano ya Bara
la Afrika ambayo yalifanyika kwa
mara ya kwanza, Februari 1957 katika
jiji la Khartoum, Sudan.
Katika mashindano haya hakukuwa na
mechi za kufuzu ambako nchi nne
waanzilishi wa CAF, Misri, Sudan,
Ethiopia na Afrika Kusini zilipanga
mahali pa kufanyika michuano hiyo.

Afrika Kusini ilifutwa katika michuano
hiyo baada ya kukataa kutuma kikosi
chenye mchanganyiko wa wachezaji
weusi na wazungu weupe hali ambayo
ilitosha kuifanya Ethiopia iende moja
kwa moja hadi hatua ya fainali.

Hali hiyo ilisababisha pia kuchezwa
mechi mbili tu hadi bingwa
kupatikana, Misri iliumana na Sudan
katika hatua ya Nusu Fainali na
kushinda na baadaye kuifunga Ethiopia
katika hatua ya fainali na kutawazwa
bingwa wa kwanza wa CAN.
Ethiopia ilikuwa icheze Nusu fainali
na Afrika Kusini ambayo iliondolewa
na hivyo kubahatika kwenda fainali
moja kwa moja.

Miaka miwili baadaye, Misri ilikuwa
mwenyeji wa mashindano hayo
yaliyofanyika katika jiji la Cairo,
ambayo pia yalizishirikisha timu zile
zile tatu na Misri ikatwaa ubingwa
kwa mara ya pili kwa kuibwaga
Sudan.

Mashindano yalizidi kupata umaarufu,
mwaka 1962 yalifanyika mjini Addis
Ababa, Ethiopia na kwa mara ya
kwanza kulikuwa na michuano ya
awali ya kufuzu kushiriki fainali hizo
ili kupata timu nne zitakazoshiriki
hatua ya fainali.

Wenyeji Ethiopia na mabingwa
watetezi Misri walifuzu moja kwa
moja na timu nyingine mbili
zilizoshiriki ni pamoja na Nigeria na
Tunisia.

Kwa mara ya tatu, Misri ilifikia hatua
ya fainali lakini safari hii iliangushwa
na Ethiopia ambayo ilitwaa taji hilo
baada ya kuibwaga, Tunisia katika
hatua ya Nusu Fainali na baadaye
kuiangusha Misri katika dakika za
nyongeza.

Ghana ambao ni wenyeji wa fainali za
CAN hapo mwakani, ilishiriki kwa
mara ya kwanza mwaka 1963 ikiwa
mwenyeji na kulibeba taji baada ya
kuibwaga Sudan, katika hatua ya
fainali.

Miaka miwili baadaye, Ghana tena
ililibeba taji hilo nchini Tunisia ikiwa
na kikosi ambacho kilijaa wachezaji
wapya huku waliotwaa taji hilo mwaka
1963 wakiwa wawili tu. Hadi hapo
Ghana ilijiwekea rekodi ya kutwaa taji
hilo mara mbili sawa na Misri.

Utaratibu wa fainali za mwaka 1968
ulibadilika kwa kujumuisha timu nane
kati ya 22 zilizoshiriki katika hatua ya
awali ya kuwania kufuzu, timu ambazo
baadaye zilifuzu nane na kupangwa
katika makundi mawili ya A na B.
Katika utaratibu huo mpya, timu mbili
zilizofanya vizuri katika kila kundi
zilisonga mbele katika hatua ya Nusu
Fainali, mfumo ambao uliendelea
kutumika hadi mwaka 1992.

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
(DRC) ilitwaa taji hilo kwa mara ya
kwanza mwaka 1968 kwa kuifunga
Ghana katika mechi ya fainali.

Katika fainali za mwaka 1968,
mshambuliaji nyota wa Ivory Coast,
Laurent Pokou aliibuka mfungaji bora
akiwa amefunga mabao sita na
kufanya hivyo tena katika fainali za
mwaka 1970 kwa kufunga mabao
manane.

Rekodi yake ya mabao 14 katika
fainali mbili imeendelea kuwa rekodi
ya kipekee katika michuano hiyo.

Fainali za mwaka 1970 zilifanyika
nchini Sudan na kwa mara ya kwanza
katika historia, fainali hizo zilianza
kuonyeshwa kwenye Televisheni huku
wenyeji wakibeba kombe hilo baada
ya kuwabwaga Ghana ambao
walikuwa wakifikia hatua hiyo kwa
mara ya nne mfululizo.

Kuanzia mwaka 1970 hadi 1980 nchi
sita zilitamba katika michuano hiyo
kwa kuibuka vinara, nchi hizo ni
Sudan, Congo Brazaville waliolibeba
mwaka 1972, Zaire (DRC) Morocco,
Ghana na Nigeria.

Zaire ilibeba kombe hilo kwa mara ya
pili mwaka 1974 (awali ililitwaa ikiwa
inatumia jina la DRC kabla ya kubadili
na kuwa Zaire na sasa kurudia jina la
DRC) baada ya kuilaza, Zambia katika
mechi ya fainali.

Mechi hiyo ya fainali ililazimika
kuchezwa mara mbili baada ya timu
hizo kutoka sare ya mabao 2-2 katika
dakika za nyongeza na kurudiwa siku
mbili zilizofuata ambako Zaire
ilishinda kwa mabao 2-0.

Katika mechi hizo, mabao yote manne
ya Zaire katika mechi hizo mbili
yalifungwa na mshambuliaji wao,
Mulamba.

Morocco kwa mara ya kwanza ilibeba
taji hilo mwaka 1976 nchini Ethiopia
wakati Ghana ililibeba taji kwa mara
ya tatu mwaka 1978 na kuwa nchi ya
kwanza kujiwekea rekodi ya kubeba
taji hilo mara tatu.

Mwaka 1980, Nigeria ilikuwa
mwenyeji wa fainali hizo ambazo pia
Tanzania ilishiriki na wenyeji Nigeria
walifanikiwa kulibakisha kombe
nyumbani baada ya kuilaza, Algeria
katika fainali.

Ghana iliendeleza ubabe mwaka 1982
kwa kulitwaa kombe nchini Libya,
ilianza kwa kuinyuka, Algeria katika
hatua ya Nusu Fainali na kuumana na
wenyeji Libya katika mechi ya fainali
kwa mikwaju ya penalti.

Miaka miwili baadaye, Cameroon
walibeba taji hilo kwa kuilaza Nigeria
na mwaka 1986 walifikia hatua ya
fainali na kuumana na Misri lakini ni
Misri ndio walioibuka vinara kwa
mikwaju ya penalti.

Mwaka 1988, nyota ya Cameroon
iling’ara baada ya kufikia hatua ya
fainali na kulibeba kombe kwa ushindi
dhidi ya Nigeria wakati mwaka 1990,
Nigeria ilianguka tena na kujikuta
ikishindwa kulibeba kombe ambalo
lilichukuliwa na Algeria.

Katika fainali za mwaka 1992, idadi ya
timu iliongezeka na kufikia 12 ambazo
ziligawanywa katika makundi manne,
kila kundi lilitoa timu mbili
zilizosonga mbele katika hatua ya
Robo Fainali.

Mchezaji mahiri wa Ghana, Abedi Pele
Ayew ambaye alifunga mabao matatu
katika fainali hizo ndiye
aliyetangazwa kuwa mwanasoka bora
wa fainali hizo kutokana na mchango
wake ulioiwezesha timu hiyo kufikia
hatua ya fainali.

Hata hivyo, katika mechi ya fainali
dhidi ya Ivory Coast alitolewa nje na
timu yake ilishindwa kufurukuta.

Utaratibu wa timu 12 uliendelea
mwaka 1994 nchini Tunisia ambako
wenyeji walijikuta wakilala katika
hatua ya kwanza na Nigeria ambao
ndio waliofikia fainali na kuibwaga
Zambia hadi kutwaa taji.

Nigeria ambayo wakati huo ilifuzu
kwa mara ya kwanza fainali za Kombe
la Dunia iliwafunga Zambia ambao
mwaka mmoja kabla ya fainali hizo
ilipatwa na msiba mkubwa wa kufiwa
na nyota wake waliokufa katika ajali
ya ndege. Rashid Yekini, mshambuliaji
wa Nigeria aliibuka kinara wa
upachikaji mabao akiwa na mabao
matano, Yekini katika fainali za
mwaka 1992 aling’ara kwa mabao
manne.

Mwaka 1996, Afrika Kusini ilikuwa
mwenyeji ikishiriki kwa mara ya
kwanza baada ya kusimamishwa
kutokana na sera za ubaguzi wa rangi
zilizokuwa zikitawala nchini humo.

Timu ziliongezwa na kufikia 16
ambazo ziligawanywa katika makundi
manne ingawa baadaye timu hizo
zilibakia 15 baada ya Nigeria kujitoa
katika hatua za mwisho kwa sababu
zilizotajwa kuwa ni za kiusalama.
Afrika Kusini ikiwa na kikosi maarufu
cha Bafana Bafana ililibakisha taji hilo
nyumbani na nahodha wa timu hiyo,
Neil Tovey akawa mzungu wa kwanza
kulibeba juu kombe hilo.

Miaka miwili baadaye fainali hizo
zilipigwa nchini Burkina Faso ambako
Afrika Kusini ilifurukuta na kukawa na
matumaini makubwa ya kulibeba taji
hilo lakini timu hiyo ilishindwa
kutamba mbele ya Misri walioibuka
vinara.

Mwaka 2000 fainali ziliandaliwa kwa
ushirikiano wa nchi za Ghana na
Nigeria ambao walichukua nafasi ya
Zimbabwe iliyoandaliwa kuwa
mwenyeji.

Cameroon ilifanikiwa kulibeba taji hilo
baada ya kuibwaga Nigeria kwa
mikwaju ya penalti.

Mambo
yaliinyookea tena Cameroon au
Indomitable Lions mwaka 2002 kwa
kuwafunga Senegal ambao walifikia
hatua ya fainali kwa mara ya kwanza
na mwaka 2004 wenyeji Tunisia
walifanikiwa kulibakisha kombe
nyumbani baada ya kuilaza, Morocco
kwa mabao 2-1.

Mwaka 2006, kombe pia lilichukuliwa
na wenyeji, Misri, ambao pia
walijiwekea rekodi ya kubeba taji hilo
kwa mara ya tano, Misri wakiwa
nyumbani mjini Cairo waliibwaga
Ivory Coast katika fainali.

Bila shaka kwa sasa anasubiriwa kwa
hamu kinara wa taji hilo kwa mwaka
2008.

Rekodi za washindi wa CAN tangu
kuanzishwa kwake…
Mwaka Nchi iliyoshinda
1957 Misri
1959 Misri
1962 Ethiopia
1963 Ghana
1965 Ghana
1968 DRC
1970 Sudan
1972 Congo Brazzaville
1974 DRC
1976 Morocco
1978 Ghana
1980 Nigeria
1982 Ghana
1984 Cameroon
1986 Misri
1988 Cameroon
1990 Algeria
1992 Ivory Coast
1994 Nigeria
1996 Afrika Kusini
1998 Misri
2000 Cameroon
2002 Cameroon
2004 Tunisia
2006 Misri
2008 misri
2010 Misri
2012 Zambia
2013 Nigeria
2015 ivory cost

 
FULU VIWANJA