Novemba 26, 2013
MECHI YA TANZANITE SASA KUCHEZWA DAR
Mechi ya kwanza ya raundi ya michuano ya
Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kwa wanawake chini ya miaka 20 kati ya
Tanzania (Tanzanite) na Afrika Kusini iliyokuwa ichezwe Mwanza sasa
itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada ya ukaguzi uliofanywa na maofisa
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imebainika uwanja huo
unatakiwa ufanyiwe marekebisho ambayo hayawezi kuwahi Desemba 7 mwaka
huu, siku ambayo ndiyo mechi hiyo inatakiwa kuchezwa.
Vyumba vya wachezaji vya uwanja huo ndilo eneo ambalo linatakiwa kufanyiwa marekebisho makubwa.
KILIMANJARO STARS YATUA SALAMA NAIROBI
Timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro
Stars) imewasili salama Nairobi, Kenya tayari kwa mashindano ya Kombe la
Chalenji yanayoanza kesho (Novemba 27 mwaka huu) katika Uwanja wa
Nyayo.
Kilimanjaro Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager iliwasili saa 3 usiku kwa ndege ya RwandAir,
na imefikia katika hoteli ya Sandton iliyoko katikati ya Jiji la
Nairobi.
Kwa mujibu wa programu ya Kocha Mkuu Kim
Poulsen, Kilimanjaro Stars leo (Novemba 26 mwaka huu) ni mapumziko
ambapo kesho itafanya mazoezi kujiandaa kwa mechi yake ya kwanza dhidi
ya Zambia itakayochezwa Novemba 28 mwaka huu Uwanja wa Machakos.
WANNE WASHINDA UCHAGUZI CECAFA
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu
Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limepata wajumbe wapya wa wanne wa
Kamati ya Utendaji katika uchaguzi uliofanya leo (Novemba 26 mwaka huu)
hoteli ya Hillpark jijini Nairobi.
Uchaguzi huo ulifuatiwa na Mkutano Mkuu
wa CECAFA ulioongozwa na Mwenyekiti wake Leodegar Tenga na kuhudhuriwa
na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF), Kalusha Bwalya na ofisa wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA), Emmanuel Maradas.
Rais wa zamani wa Shirikisho la Vyama
vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Lawrence Mulindwa ndiye aliyeongoza
katika uchaguzi huo ambapo wasimamizi walikuwa Bwalya na Maradas.
Mulindwa alipata kura zote 12 na
kufuatiwa na Tariq Atta wa Sudan (10), Abdigaani Saeb Arab wa Somalia
(9) na Raoul Gisanura wa Rwanda (8). Atta, Arab na Gisanura walikuwa
wakitetea nafasi zao.
Walioshindwa ni Rais wa Chama cha Mpira
wa Miguu Sudan Kusini (SSFA), Alei Chabor aliyepata kura tano na Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), Sam Nyamweya aliyepata
kura nne.
MICHUANO YA UHAI YAHAMIA CHAMAZI
Michuano ya Kombe la Uhai imeingia hatua
ya robo fainali ambapo sasa mechi zinachezwa kwenye Uwanja wa Azam
Complex uliopo Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Uamuzi wa kuhamisha mechi hizo kutoka viwanja vya Karume na DUCE ni kuziwezesha zote kuoneshwa moja kwa moja (live) na Azam Tv.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunaomba radhi kwa washabiki ambao watakuwa wameathirika kutokana na uamuzi huo.
USAJILI DIRISHA DOGO KUFUNGWA DESEMBA 15
Wakati dirisha dogo la usajili
linafungwa Desemba 15 mwaka huu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) tunazikumbusha klabu zote kuheshimu kanuni na kuzingatia muda
uliowekwa.
Pia tunakumbusha kuwa kupeleka mchezaji
kwa mkopo katika klabu nyingine hakutoi nafasi ya kusajili mchezaji
mpya. Kama klabu ilisaji wachezaji 30 maana yake ni kuwa haina nafasi ya
kuongeza wachezaji.
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni
(foreign players), tunakumbusha kuwa kuanzia msimu ujao 2014/2015
watakuwa watatu tu badala ya watano wa sasa.
Kuhusu usajili wa wachezaji kutoka nje
mpaka sasa hakuna hata klabu moja imeshaingia kwenye TMS kuomba
uhamisho. Itakapofika Desemba 15, system ya TMS itafunga.
RAMBIRAMBI MSIMBA WA ANDREW KILOYI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwamuzi wa zamani wa
FIFA, Andrew Kiloyi kilichotokea mjini Iringa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha
Waamuzi wa Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mahano, Kiloyi
alifariki dunia juzi (Novemba 24 mwaka huu) kutoka na ugonjwa wa fangasi
ya ubongo, na marehemu amesafirishwa kwenda kwao Kigoma ambapo
atazikwa.
Kiloyi alizaliwa Mei 5, 1968. Alijiunga
na uamuzi wa mpira wa miguu mwaka 1988 ambapo alipata beji ya FIFA mwaka
2001 akiwa mwamuzi msaidizi. Alistaafu uamuzi mwaka 2009, na hadi
anafariki akiwa mjumbe wa Kamati ya Waamuzi ya Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Iringa (IREFA).
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linatoa pole kwa familia ya marehemu, IREFA, ndugu, jamaa na
marafiki kutokana na msiba huo na kuwataka kuwa na moyo wa subira na
uvumilivu katika kipindi hicho cha majonzi. Mungu aiweka mahali pema
roho ya marehemu Kiloyi.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)