Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa
Ligi (Saa 72) iliyokutana jana Januari 4, 2018 imejadili mechi mbalimbali za
Ligi Kuu (VPL) Daraja la Kwanza (FDL) na Daraja la Pili (SDL).

LIGI KUU YA VODACOM
Mechi namba 72 (Mbeya City 0 vs
Simba 1).Kamishna wa mechi hiyo Billy Mwilima amepewa Onyo Kali kwa kuruhusu
mchezaji Hamisi Msabila wa Mbeya City kucheza mechi bila kuonyesha leseni,
hivyo kukiuka Kanuni ya 14(16 na 17) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za
Mchezo.
Mechi namba 81 (Ndanda 1 vs Njombe
Mji 1). Klabu ya Ndanda imepigwa faini ya sh 500,000 (laki tano) kwa
kutowasilisha orodha ya wachezaji wake (team match list) kwenye kikao cha
maandalizi ya mechi (pre- match meeting) kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya
14(2k) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu dhidi ya Ndanda katika
mechi hiyo iliyofanyika Novemba 24, 2017 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona
mjini Mtwara imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu.
Pia Kamati imeiomba Sekretarieti ya
Bodi ya Ligi kutoa Waraka mwingine kwa klabu kuzikumbusha kuhusu kutoa orodha
ya wachezaji kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre-match meeting).
Mechi namba 83 (Yanga 1 vs Tanzania
Prisons 1). Tanzania Prisons imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya
kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre-match meeting) ikiwa na maofisa
watatu badala ya wanne, hivyo kwenda kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Kuu
kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu dhidi ya Tanzania Prisons
katika mechi hiyo iliyochezwa Novemba 25, 2017 Uwanja wa Azam Complex ni kwa
mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu.
Wachezaji Lambart Sabiyanka wa
Tanzania Prisons na Obrey Chirwa wa Yanga wamesimamishwa kwa kuzingatia Kanuni
ya 9(5) ya Ligi Kuu kutokana na kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu,
wakisubiri malalamiko dhidi yao kusikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF.
Pia Kamati imeiomba TFF iipatie Bodi
ya Ligi uamuzi (ruling) wa Kamati ya Nidhamu juu ya mchezaji wa Yanga
kusimamishwa baada ya mechi dhidi ya Mbao FC wakati akisubiri mashtaka yake ili
kuufanyia kazi kwa ajili ya mapendekezo ya marekebisho ya Kanuni.
Mechi namba 84 (Mbao 1 vs Mwadui 0).
Klabu ya Mbao FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na
washabiki wake kuruka uzio wa ndani na kwenda kushangilia katika eneo
lisiloruhusiwa katika mechi iliyochezwa Novemba 25, 2017 Uwanja wa CCM Kirumba
jijini Mwanza.
Adhabu dhidi ya Mbao FC ni
uzingativu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 90 (Lipuli 0 vs Tanzania
Prisons 1).Mtunza Vifaa wa Lipuli FC, George Mketo amesimamishwa akisubiri
suala lake la kuwatukana waamuzi katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba 30,
2017 Uwanja wa Samora mjini Iringa kusikilizwa na Kamati ya Nidhamu. Uamuzi wa
kumsimamisha umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kuhusu Usimamizi wa Ligi.
Mechi namba 94 (Mbao 2 vs Yanga 0).
Kocha wa Mbao FC, Etiene Ndayiragije amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya
sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuondolewa kwenye mchezo (ordered off) na
Mwamuzi kwa kushindwa kuheshimu taratibu na kuonywa mara tatu.
Adhabu hiyo dhidi ya Kocha
Ndayiragije katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba 31, 2017 Uwanja wa CCM
Kirumba imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 40(11) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti
wa Makocha.
Pia klabu ya Mbao FC imepigwa faini
ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuonyeshwa kadi zaidi ya tano katika mechi
hiyo. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(10) kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 96 (Mwadui 2 vs Ruvu
Shooting 1).Klabu ya Mwadui imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya
kuonyeshwa kadi zaidi ya tano katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 1, 2018
Uwanja wa Mwadui Complex. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(10)
ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu
LIGI DARAJA LA KWANZA
Mechi namba 37 Kundi B (JKT Mlale 1
v Mufindi United 0). Klabu ya Mufindi United imepigwa faini ya sh. 500,000
(laki tano) kutokana na Kiongozi wake Hussein Turuka kutoa lugha chafu kwa
Mwamuzi katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba 31, 2017 mjini Songea. Adhabu
hiyo imezingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 40 Kundi B (Mawenzi
Market 1 v Polisi Dar 0). Klabu ya Mawenzi Market imepigwa faini ya sh. 500,000
(laki tano) kutokana na washabiki wake kutaka kuwapiga waamuzi na kuwashawishi
ball boys kuchukua mipira iliyotoka nje na kuwapelekea jukwaani. Adhabu
hiyo katika mechi hiyo iliyochezwa Desemba 31, 2017 ni kwa mujibu wa Kanuni ya
42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Pia Kocha Mkuu wa Mawenzi Market
amepewa Onyo Kali kwa kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre-macth
meeting) kwa dakika saba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi
Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 39 Kundi C (Dodoma FC 3
v Alliance Schools 2). Klabu ya Alliance Schools imepigwa faini ya sh. 300,000
(laki tatu) kwa timu yake kuonyeshwa kadi zaidi ya tano katika mechi hiyo
iliyofanyika Desemba 30, 2017 mjini Dodoma. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni
ya 42(10) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mchezaji Shaban William wa Alliance
Schools amesimamishwa, hadi suala lake la kumpiga Mwamuzi litakaposikilizwa na
Kamati ya Nidhamu ya TFF. Uamuzi wa kumsimamisha umezingatia Kanuni ya 9(5) ya
Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Usimamizi wa Ligi.
Waamuzi wote wanne; Andrew Shamba,
Abdallah Mkomwa, Athuman Athuman na Omari Juma wamefungiwa miaka mitatu kila
mmoja kwa kuchezesha mechi hiyo chini ya kiwango. Adhabu dhidi ya waamuzi hao
imezingatia Kanuni ya 38(1a) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa
Waamuzi.
Pia Kamishna wa mechi hiyo Mackshem
T. Nzunda amefungiwa miaka mitatu kwa kushindwa kutoa taarifa ya mchezo kwa
usahihi. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 39(1) ya Ligi Daraja la
Kwanza kuhusu Udhibiti wa Kamishna.
Kamati imeomba suala la waamuzi hao
ambao baadhi yao ni wa Ligi Kuu, kupitia TFF liwasilishwe kwenye chombo chenye
dhamana ya kisheria ya rushwa kufanyiwa uchunguzi zaidi.
LIGI DARAJA LA PILI
Mechi namba 18 Kundi B (Africans
Sports 1 v Kitayosce 2). Kitayosce imepigwa faini ya sh. 50,000 (elfu hamsini)
baada ya kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre-match meeting) ikiwa na
maofisa watatu badala ya wanne, hivyo kwenda kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya
Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu dhidi yao katika mechi hiyo
iliyofanyika Desemba 29, 2017 jijini Tanga imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya
14(3) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu taratibu za Mchezo.
Mechi namba 16 Kundi C (Mighty
Elephant 1 v Green Warriors 3). Kocha wa Green Warriors, Azish Kondo amefungiwa
mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kuondolewa
kwenye mchezo (ordered off) na Mwamuzi kwa kutumia lugha chafu.
Adhabu hiyo dhidi ya Kocha Kondo
katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba 29, 2017 mjini Songea imetolewa kwa
kuzingatia Kanuni ya 40(10) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa Makocha.
Mechi namba 18 Kundi C (Mkamba
Rangers 0 v Boma 1). Klabu ya Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 500,000
(laki tano) kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani (pitch). Adhabu
hiyo katika mechi hiyo iliyochezwa Desemba 29, 2017 ni kwa mujibu wa Kanuni ya
42(1) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 16 Kundi D (Area C v
Nyanza). Timu ya Nyanza FC imeshushwa madaraja mawili na matokeo ya michezo
yako yote imefutwa kwa kutofika uwanjani bila kutoa sababu yoyote na
kusababisha mechi yao dhidi ya Area C iliyokuwa ichezwe Desemba 29, 2017 mjini
Dodoma isifanyike.
Uamuzi huo dhidi ya Nyanza FC
umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 28(1) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Kutofika
Uwanjani. Pia kwa mujibu wa Kanuni ya 28(2) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu
Kutofika Uwanjani, imepigwa faini ya sh. 2,000,000 (milioni mbili) ambapo sh.
1,000,000 (milioni moja) itachukuliwa na Bodi ya Ligi, na sh. 1,000,000
(milioni moja) italipwa timu pinzani.
Vilevile Kamati imeiomba
Sekretarieti kukiandikia barua Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Manyara (MARFA)
ili kujua tatizo la timu hiyo.
MECHI YA MVUVUMWA VS FRIENDS RANGERS
Kamati imeipa Friends Rangers
ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Mvuvumwa kuchezesha wachezaji
ambao hawajasajiliwa (non qualified) katika mechi ya Kundi A Ligi Daraja la
Kwanza (FDL) kati ya timu hizo iliyochezwa Oktoba 29, 2017. Mvuvumwa ilishinda
mechi hiyo mabao 4-1.
Uamuzi huo dhidi ya Mvuvumwa
umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(18) na 42(20) za Ligi Daraja la Kwanza.
Nayo Friends Rangers imepewa ushindi kwa kuzingatia Kanuni ya 14(37) na ya Ligi
Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
Vilevile viongozi wa Mvuvumwa
waliohusika kughushi leseni zilizotumiwa na wachezaji hao ambao hawakusajiliwa
watafikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi.
MALALAMIKO YA ALLIANCE SCHOOLS
Kamati imepitia malalamiko ya
Alliance Schools kupinga uchezeshaji wa Mwamuzi wa mechi yao dhidi ya Dodoma FC
iliyofanyika Desemba 30, 2017 Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Baada ya kupitia hoja zote, Kamati
haikukubaliana na malalamiko hayo kwa vile hayakuwa na vielelezo wala kanuni za
kuyathibitisha. Pia kwa suala la muda, Kamati imejiridhisha kuwa kazi ya
kutunza muda ni ya Mwamuzi.