Siku 50 kuelekea kikomo cha mkataba wake na klabu ya Mtibwa Sugar, mlinzi wa kati na nahodha wa timu hiyo bingwa mara mbili wa zamani wa Tanzania Bara, Salim Mbonde ameweka wazi kuwa anaweza kujiunga na klabu yoyote kubwa nchini baada ya misimu mitatu ya kujijenga na kujiendeleza chini ya kocha Mecky Mexime.
Mbonde alijiunga na Mtibwa kama mchezaji wa timu B misimu mitatu iliyopita akitokea JKT Oljoro ya Arusha tayari ameiwakilisha timu ya Taifa ya Tanzania ( Taifa Stars) katika michezo minne, huku pia akicheza mara mbili katika timu ya bara (Kilimanjaro Stars).

Mchezaji huyo wa nafasi ya beki ya kati hajaitwa katika timu ya taifa ambayo itacheza na Chad katika mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2017.
Nimefanya mahojiano na mlinzi huyu mwenye umbo kubwa, pamoja na kuzungumzia mkataba wake wa sasa na hatma katika timu yake, Mbonde amezungumzia pia namna alivyowatosa Simba SC misimu miwili iliyopita baada ya timu hiyo kutaka kumuhamisha kinyume na utaratibu akiwa na mkataba na Mtibwa.