PICHA inayomuonesha Rais wa wakati
huo wa Sudan, Jaafar El Nimeiry
akisalimiana na wachezaji wetu
waliokuwa vifua wazi, ni picha
maarufu sana kwenye sehemu
mbalimbali ikiwemo humu
lakini si
wengi wanaifahamu hadithi inayohusu
tukio hilo la mwaka 1972, miaka 41
iliyopita.
Kwa kutoifahamu hadithi hiyo, kuna
baadhi ya Watanzania kwenye
mitandao kadhaa ya kijamii
wamewahi kuijadili picha hiyo katika
mtazamo wa jinsi Tanzania
ilivyokuwa bado nyuma kimaendeleo
kiasi cha wachezaji wake kucheza
bila jezi, wakidhani hiyo ilikuwa ni
hali ya kawaida miaka hiyo. Si kweli.
Jezi zimevaliwa nchini mwetu tangu
klabu ya kwanza ya soka kuundwa
ambayo ni African Sports ya Zanzibar
kwenye miaka ya 1920, miaka 52
kabla ya tukio la picha hii ya vifua
wazi.
Ukiitazama picha hiyo, unamuona
nahodha wa timu yetu ya Taifa wa
miaka hiyo,kiungo mahiri
Abdulrahman Juma, mzaliwa wa
Kondoa, mkoani Dodoma ambaye pia
alikuwa nahodha wa timu ya mkoa wa
Pwani uliojumuisha Dar es Salaam
miaka ile na pia alikuwa nahodha wa
timu yake aliyokuwa akiichezea ya
Yanga. Hapo anaonekana
akimtambulisha Rais Nimeiry kwa
wachezaji wa Tanzania
. Kwa sasa
mchezaji huyo mkali kwa kuchonga
kona ni marehemu.
Aliyeshikana mkono na Rais Nimeiry
ni Omar Zimbwe wa African Sports ya
Tanga. Huyu alikuwa ni beki wa kati
kisiki ambaye alikuwa maarufu kwa
kupiga penalti. Wa kwanza kushoto
ni Mohammed Chuma ambaye alipewa
jina la “Chuma” lililomnata na kuwa
lake rasmi kutokana na ugumu wake
kama chuma katika kupitwa na
washambuliaji. Jina lake halisi ni
Mohammed Ali.
Beki huyo wa kushoto alichezea timu
ya Taifa mfululizo kuanzia mwaka
1964 mpaka mwaka 1975 alipostaafu
kuichezea timu hiyo na kubaki
kuichezea timu yake ya Nyota ya
Mtwara. Alifanyiwa sherehe kubwa ya
kustaafu iliyojumuisha mechi baina ya
Tanzania na Kenya na kuzawadiwa
vya kutosha. Chuma, mzaliwa wa
Mtwara, naye ni marehemu.
Kulia kwa Abdulrahman Juma na
kushoto kwa Zimbwe ni Kitwana
Manara “Poppat” wa Yanga aliyekuwa
mkali wa kufunga mabao hasa ya
kichwa na hasa hasa ya kona za
Abdulrahman Juma. Kitwana alikuwa
mshambuliaji wa kati ambapo, kwa
mfumo wa enzi hizo, alikuwa namba
tisa. Ana asili ya mkoa wa Kigoma
lakini ni mkazi wa Dar es Salaam
tangu enzi hizo. Alianza soka akiwa
kipa akamaliza akiwa mfumania
nyavu.
Uso unaoonekana kati kati ya
Abdulrahman Juma na Rais Nimeiry ni
wa Mshambuliaji matata wa wakati
huo, Abdallah Kibaden aliyekuwa
namba 10. Kwa sasa Kibaden ni kocha
wa Kagera Sugar ya Bukoba. Ni
mzaliwa wa Dar es Salaam.
Waliobaki
pichani wameshindwa kutambulika
kutokana na sura zao kutoonekana
lakini mwenye jezi anayeonekana
kipande mwisho kulia anaweza kuwa
kipa Omar Mahadhi wa African Sports
ya Tanga wakati huo kwa sababu kipa
huyo aliingia uwanjani siku hiyo akiwa
amevaa jezi.
Mahadhi, ambaye kwa sasa ni
marehemu, alikuwa kipa namba moja
wa Tanzania kuanzia mwaka 1971
alipoibuka kwenye timu ya “Taifa Cup”
ya mkoa wa Tanga. Aliichezea timu ya
taifa mfululizo mpaka mwaka 1978.
Sifa ya Mahadhi ilikuwa uwezo wa
kucheza vizuri akiwa golini na akiwa
mshambuliaji.
Akicheza kama
mshambuliaji, hasa kwenye timu yake
ya African Sports na timu ya mkoa wa
Tanga, alikuwa hatoki bila kutikisa
nyavu!
Hakucheza mbele akiwa timu ya Taifa
na akichezea Simba aliyojiunga nayo
mwaka 1975 mwishoni.
Akiwa kipa wa
timu ya Taifa, aliwahi mwaka 1975
kupiga mpira uliojaa wavuni kwenye
lango la Kenya lakini mwamuzi
alikosea kwa kuamuru ipigwe kona
kuelekea Kenya. Sunday Manara
(Yanga) alipiga kona hiyo na Gibson
Sembuli (Yanga) alifunga bao.
Kuhusu picha hii maarufu, mwaka
1972, liliandaliwa tamasha la soka
kusherehekea miaka 18 ya chama cha
TANU (Tanganyika African National
Union) kilichoanzishwa Tanganyika
Julai 7, 1954. Chama hicho kiliungana
na ASP (Afro-Shiraz Party) ya
visiwani na kuzaliwa CCM (Chama
cha Mapinduzi) Februari 5, 1977.
Tamasha hilo la shereha ya Saba Saba
1972 lilihusisha timu za Taifa za
Tanzania, Sudan na Nigeria. Mechi ya
kwanza ya tamasha hilo ilikuwa
inayohusu picha hii ya historia.
Ilikuwa ni mechi baina ya Tanzania na
Sudan. Siku hiyo hapo uwanjani
kulikuwa na marais wawili, mgeni
Nimeiry wa Sudan na mwenyeji
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
wa Tanzania, Nimeiry akawa mgeni
rasmi.
Wakati timu zinakaguliwa,
Nyerere alikuwa jukwaani.
Sasa timu zilipoingia uwanjani,
wachezaji wa Sudan wakawa safi na
jezi zao lakini wa Tanzania wakaingia
na bukta, soksi na viatu bila fulana za
juu isipokuwa kipa Mahadhi aliyevaa
jezi kamili. Watu walipigwa butwaa na
kufadhaika ambapo aliyefadhaika
zaidi alikuwa Mwalimu Nyerere
aliyekiita kitendo hicho kama timu ya
nchi yake kuingia uwanjani uchi!
Aliagiza apewe maelezo mapema
kuhusu aibu hiyo.
Baadaye, wachezaji hao waliingia
vyumbani na walipotoka walikuwa
wamevaa jezi na kucheza wakiwa
wamevaa jezi. Kumbe kilichotokea ni
kwamba jezi walizotakiwa wavae
zilifuliwa na zilikuwa hazijakauka,
huku timu zikiwa zimeitwa uwanjani.
Hatua kali ilichukuliwa baadaye kwa
waliohusika na uzembe huo
uliotusababishia aibu huku Mwalimu
Nyerere akiapa kutohudhuria tena
uwanjani kutokana na kudhalilishwa
huko.
Hata hivyo, miaka mitatu baadaye,
yaani mwaka 1975, alipobembelezwa
sana alihudhuria mechi ya Tanzania
na Ethiopia ya kutafuta nafasi ya
kucheza fainali ya mataifa ya Afrika
mwaka 1976. Alitoa angalizo kwamba
ukitokea udhalilishwaji mwingine,
siku hiyo ingekuwa mwisho kwa yeye
kuingia uwanjani kutazama mpira.
Kwa bahati mbaya sana, akiwa
jukwaani siku hiyo, ulitokea ugomvi
mkubwa wa wachezaji kupigana!
Mwalimu aliondoka wakati huo huo na
kuapa asingehudhuria tena uwanjani
kushuhudia mechi ya soka kwani
ameshuhudia kero kubwa mara mbili.
Kufuatia fujo hizo, Ethiopia iliomba
radhi kwani kipa wake ndiye
alianzisha ugomvi huo. Matukio kama
hayo yalikuwa ya kawaida miaka ile
kwa wepesi wa kanuni dhidi ya
matukio hayo.
Tukirudi kwenye mechi ya Tanzania
na Sudan, matokeo ya mechi hiyo
yalikuwa ushindi wa 3-0 kwa timu
yetu, Kibaden akifunga bao la tatu kwa
“counter attack” baada ya Mahadhi
kudaka mpira wa shambulio la Sudan
na kumrushia Kibaden aliyekimbia nao
mpaka kuuweka kambani. Kwenye
mechi yetu dhidi ya Nigeria,matokeo
yalikuwa suluhu, yaani 0-0.
Katika tamasha hilo timu yetu ilikuwa
hivi:- kipa Mahadhi (African Sports,
Tanga), beki kulia Mweri Simba
(Tanga), beki kushoto Chuma (Nyota
Mtwara),Namba nne Hassan Gobbos
(Yanga), beki tano Zimbwe (African
Sports, Tanga), Kiungo namba sita,
Nahodha Abdulrahman Juma (Yanga),
wingi ya kulia Willy Mwaijibe
(Simba), kiungo namba nane Sunday
Manara (Yanga), namba tisa Kitwana
Manara (Yanga), namba 10, Kibaden
(Simba) na wingi ya kushoto Nassor
Mashoto (Zanzibar).
Akiba: kipa Elias Michael (Yanga),
kiungo Mohammed Msomali
(Cosmopolitan), Winga Kassim Manga
(Morogoro), namba 10 Gibson Sembuli
(Yanga) na wengine wachache. Kocha;
Paul West Gwivaha.
Hii ndiyo hadithi ya vifua wazi
vya timu yetu ya taifa ya mwaka 1972.