
Anelka amepewa Adhabu ya kufungiwa Mechi 5 na kumpiga Faini £80,000 kwa kutumia Saluti hiyo inayoitwa 'Quenelle'.
Pamoja na Adhabu hizo, pia Straika huyo kutoka Ufaransa ametakiwa kuhudhuria Elimu ya Lazima.
Anelka, mwenye Miaka 34, alikana kwamba 'Quenelle' ni ya Kibaguzi na kudai Saluti hiyo ni kupinga Serikali.
Mara baada ya Adhabu hizo za FA, Klabu
yake, West Brom, imeamua kumsimamisha hadi hapo Rufaa yake na Uchunguzi
ndani ya Klabu kukamilika.
Hata hivyo, Adhabu zake zitasimamishwa ikiwa ataamua kukata Rufaa.
Anelka atapewa Siku 7 tangu atakapopata kwa Maandishi sababu za kuadhibiwa kwake za kukata Rufaa ikiwa atapenda.
Mbali ya Adhabu zake, Anelka pia ametakiwa kulipa Gharama za Uendeshwaji wa Kesi yake.
Sakata la Anelka lilianza Desemba 28
wakati akishangilia Goli lake Timu yake, West Bromwich Albion, ilipotoka
Sare 3-3 na West Ham, kwa kutumia ishara ya Saluti ambayo inahusishwa
na Mafashisti wa Nazi.
Saluti hiyo [Pichani] ambayo Mkono wake
wa kushoto aliupitisha Kifuani na Mkono wa Kulia kuelekezwa chini
huchukuliwa kama Saluti ya Nazi kwa kinyume lakini mwenyewe Anelka
amekiri hiyo inaitwa ‘Quenelle’ ili kumsapoti Rafiki yake wa France,
Dieudonné M'Bala M'Bala, ambae ni Mchekeshaji, anaesakamwa Nchini humo
kwa kuwa Mbaguzi.
Saluti hiyo ya Anelka imezua kizaazaa
kikubwa huko Ufaransa kiasi ambacho Waziri wa Michezo Nchini humo,
Valérie Fourneyron, amesema inatia kinyaa.
Anelka alitumia hiyo ‘Quenelle’
akisheherekea Bao lake la Kwanza kati ya mawili iliyofunga kwenye Sare
hiyo ya 3-3 kati ya Timu yake West Brom na West Ham na hilo likiwa Bao
lake la Kwanza kwa Klabu hiyo tangu ajiunge nayo mwanzoni mwa Msimu.
Lakini Anelka si Mwanasoka wa kwanza
kupigwa Picha akitoa hiyo ‘Quenelle’ kwani Samir Nasri wa Manchester
City na Mamadou Sakho wa Liverpool walishanaswa wakiwa pamoja na
Dieudonné wakitoa Saluti hiyo ingawa Sakho baadae alisisitiza hakujua
maana yake na alihadaiwa kuitumia.