TOMAS ROSICKY KUBAKI ARSENAL LAKINI MORATA KUTONASWA!
Meneja wa Arsenal Arsene Wenger
amethibitisha kubaki kwa Tomas Rosicky hadi mwishoni mwa Msimu lakini
pia amepuuza taarifa zilizozagaa za kumchukua Chipukizi wa Real Madrid,
Álvaro Morata, kwa Mkopo.
Rosicky, mwenye Miaka 33 na ambae
Mkataba wake unamalizika mwishoni mwa Msimu, amesema yeye anataka kubaki
Emirates hadi anastaafu lakini hadi sasa si Wenger wala Klabu
iliyothibitisha kumwongezea Mkataba.
Huu ni Msimu wa 8 kwa Rosicky kuwa Arsenal lakini Majeruhi ya mara kwa mara yamemfanya acheze Mechi za Ligi 92 tu.
Wakati huo huo, Wenger amepuuza habari
zilizozagaa kuwa Arsenal inataka kumchukua kwa Mkopo Chipukizi wa Real
Madrid, Álvaro Morata mwenye Umri wa Miaka 21.
Habari hizi zilishika hatamu mara baada
ya Juzi kuthibitishwa kuwa Theo Walcott atakuwa nje Msimu wote uliobaki
baada ya kuumia vibaya Goti.
Lakini, hapo Jana, mara baada ya Real
Madrid kuifunga Bao 2-0 Osasuna kwenye Mechi ya Copa del Rey ambayo
Morata aliingizwa mwishoni kutoka Benchi, Meneja wa Real, Carlo
Ancelotti, amesema hana nia ya kumwachia Morata kwenda nje kwa Mkopo.