STRAIKA wa Tottenham na England Jermain Defoe amekubali kujiunga na Klabu ya MLS, Major League Soccer, Toronto FC.
Defoe, mwenye Miaka 31, atajiunga na Klabu hiyo ya Canada inayocheza Ligi ya Marekani, MLS, Februari 28.
Defoe, ambae ameichezea Tottenham Mechi
250, Msimu huu amekuwa hana namba ya kudumu na mara nyingi Meneja
alietimuliwa, Andre Villas-Boas, alikuwa akimpiga Benchi na kumchezesha
Roberto Soldado na hali hii haikubadilika hata baada ya kuwekwa Meneja
mpya Tim Sherwood ambae huwachezesha Emmanuel Adebayor na Soldado.
TOTTENHAM
WAFUNGAJI BORA:
-Jimmy Greaves - 266
-Bobby Smith - 208
-Martin Chivers 174
-Cliff Jones - 159
-Jermain Defoe - 142
Defoe amesaini Mkataba wa Miaka minne na
Toronto FC lakini yuko huru kuichezea Tottenham hadi Februari 28 na
hivyo Mechi yake ya mwisho White Hart Lane inaweza kuwa ile ya EUROPA
LIGI dhidi ya Dnipro hapo Februari 27.
Defoe, aliejiunga na Spurs Mwaka 2004
akitokea West Ham, ndie Mfungaji Bora wa Pili kwenye EUROPA LIGI Msimu
huu akiwa na Bao 7 ikiwa ni Bao 1 tu nyuma ya Paulo Henrique wa
Trabzonspor.
Akiwa na England, Defoe amecheza Mechi 55 na kufunga Bao 19.