DAVID
MOYES amethibitisha kuwa Straika wake Wayne Rooney amepumzishwa kwa
kupelekwa Nchi ya Joto ili kuharakisha kwake kupona Nyonga lakini yeye
mwenyewe sasa kuonja ‘Joto la Jiwe’ toka kwa FA ambayo leo imeamua
kumfungulia Mashitaka kwa kauli yake: ‘Sasa tunacheza dhidi ya Marefa
pamoja na Wapinzani.’
Akithibitisha Rooney na Robin van Persie
kukosekana kwa Mechi ya Ligi Kuu England itakayochezwa Jumamosi Old
Trafford dhidi ya Swansea City, Meneja wa Manchester United, David
Moyes, amesema: “Tumempeleka Rooney kwenye Likizo ya Mazoezi Nchi ya
Joto. Atakuwa pamoja na Kocha wa Viungo. Yuko pamoja na Familia yake na
tunategemea atakuwa fiti kwa Mechi na Chelsea.”
Man United itasafiri kwenda Stamford Brige Jumapili Januari 19 kucheza Mechi ya Ligi na Chelsea.
Rooney amezikosa Mechi za Man United
dhidi ya Swansea na Sunderland na Van Persie hajacheza Mechi tangu
Desemba 7, na kabla ya hapo alikuwa hajacheza tangu katikati ya Novemba
lakini tangu Alhamisi amerudi kwenye Mazoezi kamili.
WAKATI HUO HUO, David Moyes amefunguliwa
Mashitaka na FA, Chama cha Soka cha England, akishitakiwa kwa Utovu wa
Nidhamu kufuatia kauli yake mara baada ya kufungwa na Sunderland 2-1
Jumanne iliyopita kwenye Mechi ya Kwanza ya Nusu Fainali ya Capital One
Cup alipodai Timu yake sasa ‘inacheza dhidi ya Marefa’ pamoja na
Wapinzani.
Baada ya Mechi hiyo, Moyes alidai: “Sasa inabidi tucheze dhidi ya Marefa na Timu pinzani. Ni mbaya sana. Tumeanza kuwacheka. ”
Kilichomkera Moyes ni Refa Andre
Marriner kutoashiria Penati lakini aliitoa baada ya ushauri kutoka kwa
Mshika Kibendera wake kufuatia Adam Johnson wa Sunderland kuanguka
wakati akikabiliana na Tom Cleverley na Moyes kuhoji: “Itakuwaje Mshika
Kibendera atoe Penati? Refa alikuwa akiangalia moja kwa moja tukio lile
lakini Mshika Kibendera alikuwa haoni kwani kazibwa na Evra! Mchezaji
wetu sisi alipewa Kadi kwa tukio kama hilo walilopewa Penati! Hata lile
Bao la kwanza ile haikuwa Frikiki ingawa ni kosa letu kutojilinda vizuri
kwa Frikiki ile na kuruhusu Bao!”
Moyes amepewa hadi Jumatano Desemba 15 Saa 3 Usiku kujibu Shitaka lake.
Mapema Wiki hii, Meneja wa Liverpool,
Brendan Rodgers, alipigwa Faini £8,000 kwa kuhoji kuhusu Refa Lee Mason
walipofungwa na Manchester City.