Social Icons

Pages

Wednesday, 15 January 2014

HENRY JOSEPH ANAPOSHINDWA KUWA MFANO MZURI KWA CHIPUKIZI SIMBA SC

KIUNGO Henry Joseph Shindika amesusa kujiunga na timu yake, Simba SC kwa sababu anaidai sehemu ya fedha zake za usajili katika Mkataba wa mwaka mmoja.
Henry alikosekana katika kikosi cha Simba SC kilichoshiriki Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar mwezi huu na kushika nafasi ya pili baada ya kufungwa 1-0 na KCC ya Uganda kwenye Fainali juzi, Uwanja wa Amaan.
Maana yake mchango wake ulikosekana, kwa sababu anadai fedha ambazo Simba SC haijakataa kumlipa na hata ikitaka kumnyima haki yake, kwa mfumo wa uendeshwaji wa soka yetu kwa sasa, hawataweza. Lazima watamlipa haki yake.


Hakuna asiyefahamu kwamba Simba SC kwa sasa ipo katika wakati mgumu, kwanza kutokana na mgogoro wa uongozi unaoendelea na pia kung’atuka kwa viongozi wawili wa Sekretarieti, Katibu Evodius Mtawala na Ofisa Habari, Ezekiel Kamwaga.
Wachezaji wa Simba SC wametimiza miezi miwili bila kulipwa mishahara, lakini ukiondoa Henry wengine wote wenye kudai fedha za usajili na mishahara walikwenda Zanzibar kuitumikia timu.
Hao waliokwenda Zanzibar uongozi utawalipa mishahara yao kwa sababu walikuwa kazini na wenye madai mengine pia miongoni mwao, watalipwa. Lakini Henry kwa kuwa hakuitumikia timu karibu nusu ya mwezi Desemba na mgomo wake unaendelea hadi Januari ikielekea ukingoni, anastahili nini?
Kitendo anachofanya Henry Joseph huwezi kukipa tafsiri nyingine, zaidi ya kukiita ni utovu wa nidhamu, kwa sababu, anazungumza na viongozi wanamuomba, avumulie atapewa, lakini yeye anagoma kwenda kambini.
Henry tayari ameingia kwenye orodha ya wachezaji wakubwa kuwahi kutokea Tanzania akiwa amewahi kucheza soka ya kulipwa, tena katika Ligi Kuu ya Ulaya, klabu ya Kongsvinger ya Nowray, hivyo anapaswa kuwa mfano bora kwa wengine.
Wachezaji wa Uganda wana desturi moja nzuri, naipenda, wanapopata nafasi ya kwenda kucheza nje ya nchi yao, mambo yakiwaharibikia, wanarejea kwenye klabu zao kucheza kwa masharti mepesi tu ili kujipanga upya.
Joseph Owino alitoka Uganda akaja Simba SC mwaka 2010 akafanya vizuri kwa misimu miwili kabla ya kuumia goti na kuwa nje kwa msimu mzima, kisha akasajiliwa Azam FC. Lakini Azam nayo ikaona beki huyo soka basi tena, ikamtema.
Owino akarejea URA iliyomuibua akacheza na hatimaye Simba SC wakaridhika naye na kumsajili tena. Haikuwa tabu Owino kuhama URA kurejea Simba SC, kwa sababu alikuwa anacheza kwa masharti nafuu.
Ni wengi tu, hata ambao wanapoteza nafasi Ulaya, hurejea Uganda kujipanga upya na huchezea klabu zao kwa masharti nafuu.  Hata baadhi ya wachezaji wa Tanzania kama Danny Mrwanda na Nizar Khalfan wamekwishawahi kupata nafasi nje, wakapoteza lakini wakarejea nyumbani kujipanga upya wakicheza kwa mashari nafuu, hatimaye wakafanikiwa tena kurejea nje.
Kwa pamoja Mrwanda na Nizar waliwahi kununuliwa na Al Tadhamon ya Kuwait, lakini baada ya msimu mmoja wakatemwa. Mrwanda alirejea Simba SC na Nizar akaenda Moro United. Nizar akapata nafasi ya kwenda kucheza Marekani na Mrwanda Vietnam.
Mbwana Samatta alisajiliwa Simba SC kwa ahadi ya fedha na gari mwaka 2011, lakini kutoakana na kucheleweshewa fungu la usajili, akagoma kujiunga na timu hiyo na kuamua kulala nyumbani mzunguko wote wa kwanza wa Ligi Kuu. 
Watu wakamshauri, naye akaelewa, Samatta akaenda kujiunga na Simba SC na katika mzunguko wa pili akang’ara sana hadi Ligi ya mabingwa Afrika, hatimaye TP Mazembe ya DRC ikamsajili kwa dau kubwa na mshahara mnono na anaendelea kucheza timu hiyo.
Henry ni mchezaji ambaye umri umeenda, tulitarajia angetambua hilo na kusaka nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza Simba SC ili aonekane na labda angerudi Ulaya. 
Hakika Henry hapaswi kuendeleza mgomo, arejee kikosini, kwani kufanya hivyo kunamuondolea sifa ya kuwa mfano bora kwa chipukizi wa timu hiyo. Jumatano njema.
 
FULU VIWANJA