Kocha Mkuu
mpya wa Yanga, Hans van Der Pluijm, raia wa Uholanzi, amesema anataka soka la
kasi huku kikosi chake kikicheza kwa ushirikiano katika kushambulia na kukaba.
Van Der
Pluijim (64), amemueleza mmoja wa viongozi wa Yanga kwamba ana imani siku
chache atakazokaa na timu nchini Uturuki, atafanya mabadiliko huku akiahidi
kuwatumia Mrisho Ngassa, Emmanuel Okwi na Simon Msuva katika aina ya ushambuliaji
wa kasi anaoutaka.
“Kocha kasema anapenda soka la kasi,
tumemueleza kuhusu wachezaji kadhaa wenye aina hiyo, amefurahia. Unajua alitaka
kujua baadhi ya mambo, mfano alitaka kujua kama tuna wachezaji wenye kasi,
tumemtajia Ngassa, Okwi, Msuva na amesema pia anataka timu inayocheza kwa
ushirikiano. Lakini naamini ataanza na safu ya ulinzi,” alisema kiongozi huyo.
“Ana mambo
mengi anataka kufanya, lakini ametaka kwanza kuiona timu, vizuri atawaona
wakicheza mechi kwa kuwa atafika kesho (leo), halafu saa chache watacheza mechi.
Atapata nafasi ya kuwaona.”
Kocha huyo
Mholanzi, amekuwa akisifiwa kwa soka la nguvu wakati akiifundisha Berekum
Chelsea ya Ghana na alipofanya mahojiano mafupi na waandishi
alisisitiza suala la subira.
