MSHAMBULIAJI
wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu amesema kwamba
ndoto za kuhamia Ulaya zinakaribia kutimia, kwani ana ofa nyingi kutoka
nchi mbalimbali, zikiwemo Hispania, Ufaransa, Ubelgiji na Italia.
Ulimwengu aliye kwenye kikosi cha Bara,
Kilimanjaro Stars kinachoshirki Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na
Kati, CECAFA Challenge amesema kwamba ana matumaini makubwa ya kuhamia
Ulaya.
“Nina
ofa nyingi na zinafanyiwa kazi kwa sasa, nadhani muda si mrefu
nitaondoka Afrika, tuombe Mungu,”alisema mshambuliaji huyo wa Tout
Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ulimwengu
anacheza klabu moja na Mtanzania, mwenzake Mbwana Ally Samatta, TP
Mazembe na wote kwa sasa ndiyo wachezaji wakubwa zaidi na tegemeo wa
Tanzania.
Wawili
hao waliwasili juzi mjini hapa wakitokea DRC, ambako waliichezea klabu
yao Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kufungwa jumla ya mabao 3-2
na Sfaxien ya Tunisia. Walifungwa 2-0 ugenini na wakashinda 2-1
nyumbani.
Jana
waliichezea Stars mechi ya kwanza ya Challenge dhidi ya Burundi na
wakaisaidia kushinda 1-0, bao la Mbwana Samatta pasi ya Mrisho Ngassa.
Walikosa bahati tu ya kufunga mabao zaidi, lakini walipata nafasi za
kutosha jana Uwanja wa Afraha, Nakuru.
Kwa kuwa Stars imefanikiwa kuingia Robo Fainali, Samatta na Ulimwengu wanatarajiwa kufanya vitu zaidi katika mashindano haya.