MWENYEKITI
wa Kamati ya Usajili ya Yanga SC, Abdallah Ahmed Bin Kleb amesema
kwamba ni vigumu kwao kumsajili mshambuliji Emmanuel Okwi wa Uganda kwa
sababu ya sakata lake na klabu yake ya zamani Simba SC.
Na
kuhusu Dan Sserunkuma, Bin Kleb amesema mchezaji huyo aling’ara katika
mechi moja ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA
Challenge dhidi ya timu dhaifu, Eritrea nchini Kenya, hivyo
hawajajiridhisha juu ya ubora wake.
“Katika
mechi na Eritrea Sserunkuma alitoa pasi za mabao yote na akasababisha
penalti ya bao lingine, Uganda ikashinda 3-0. Lakini ni mapema sana
kumfikiria kumsajili, labda tumuone kwenye hatua zijazo akiendelea
kufanya vizuri, tutamfikiria, ila kwa sasa hatujafanya lolote,”alisema
Bin Kleb.
Kleb
alisema jana alikuwa kwenye mazoezi ya timu yao, Yanga Uwanja wa Bora
Kijitonyama, Dar es Salaam na akajionea namna wachezaji wao
wanavyojituma mazoezini na kuonyesha ubora wao.
“Tulikuwepo
Kamati nzima ua Usajili, mimi Seif Magari, Mussa Katabro na Isaac
Chanji, kwa kweli wachezaji wote wanajituma sana, huu ni mtihani, kweli
tunahitaji kuongeza mshambuliaji mmoja kwa ajili ya michuano ya Afrika,
lakini awe mshambuliaji kweli, kuliko kujaza nafasi tu, tuko makini mno
katika hilo,”alisema.
Kuhusu
Okwi, Kleb alisema ni vigumu mno kumsajili kutokana na sakata la klabu
yake zamani, Simba SC na Etoile du Sahel ya Tunisia.
“Huyo
mchezaji (Okwi) kwa kweli ile hata kurudi kucheza Uganda (SC Villa)
ilikuwa bahati sana, sakata lake ni zito sana, lazima kwanza Simba SC
walipwe fedha zao (dola za Kimarekani 300,000),”alisema.
Pamoja na hayo, Bin Kleb amesema anaridhishwa na viwango vya wachezaji wao waliopo Challenge katika timu mbalimbali.
Katika
kikosi cha Rwanda, Yanga inaye Haruna Niyonzima, Uganda Hamisi Kiiza na
Tanzania Bara Deo Munishi ‘Dida’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Athumani
Iddi ‘Chuji’, Hassan Dilunga na Mrisho Ngassa.