WAMEIBOMOA Gor Mahia. Ndivyo unavyoweza
kusema kuhusiana na hatua ya Simba ya Tanzania kuwasajili kipa, Ivo
Mapunda na beki Donaldi Musoti.
Klabu hiyo ya Tanzania ambayo maofisa
wake walikuwapo jijini Nairobi wakati wa mashindano ya Cecafa Senior
Challenge Cup yaliyomalizika juzi Alhamisi, walikamilisha usajili wa
wawili hao jana Ijumaa.
Mapunda aling’ara katika michuano hiyo
akiwa na timu ya Tanzania Bara, wakati Musoti alikuwa katika kikosi cha
Kenya. Mapunda amesaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu wakati Musoti
amesaini miaka miwili.
Musoti alisema: “Nimefurahi sana kusaini
Simba, nakwenda kufanya kazi na Loga (Zdravko Logarusic) ambaye nimekaa
naye Gor Mahia kwa mafanikio.
“Nina uzoefu wa kutosha na soka la
Afrika Mashariki na ninadhani nitafanya kazi nzuri na Simba kama Wakenya
wenzangu waliopita, kikubwa ni ushirikiano tu.”
Katika kikosi cha Gor Mahia,Musoti hucheza sambamba na Ivan Anguyo au Edwin Lavatsa.
Makamu Mwenyekiti wa Kwanza wa Gor
Mahia, Faz Ochieng, amekiri kuwa kuondoka kwa wawili hao ni pigo kwao na
watakaa kujadiliana nini cha kufanya.
“Sijapata taarifa rasmi za kuondoka
kwao, lakini mikataba yao inamalizika mwezi huu na ilikuwa tukae nao
kujadiliana juu ya mikataba mipya,” alisema.
Gor Mahia itakuwa imepata pigo kubwa
baada ya wachezaji hao kusaini Simba kwani walikuwa tegemeo kwao na
waliibeba kwenye Ligi Kuu Kenya msimu uliomalizika ambapo timu hiyo
ilitwaa ubingwa.
Mapema wiki hii matajiri wa Gor Mahia
walijinadi kuwa watahakikisha kwa gharama yoyote ile wanawabakiza
wachezaji hao jambo ambalo limegonga mwamba kwani viongozi wa Simba
waliowasili usiku wa Jumanne iliyopita wameshamaliza kazi.
Kuthibitisha jinsi klabu hiyo ilivyopata
pigo, baadhi ya mashabiki wa Gor Mahia jana Ijumaa walivamia ofisi za
timu hiyo zilizopo maeneo ya uwanja wa soka wa Nyayo wakiwa na
mavuvuzela na kuwapigia kelele viongozi wao wakiwahoji imekuwaje
wamewaachia wawili hao kujiunga na Simba.
Mashabiki hao waliokuwa zaidi ya 50
wamechukizwa na jambo hilo na kuwaoana viongozi wao ni wazembe kwani
klabu hiyo ni kubwana ina fedha za kuwabakiza.
