WAKATI
Andre Villas-Boas akikiri Tottenham wamepata kipondo kikubwa toka
Manchester City cha 6-0 kwa sababu ya uchezaji wao mbovu, David Moyes
amesikitishwa na Difensi ya Manchester United iliyoruhusu Bao la Dakika
ya 90 na kuipa Cardiff City Sare ya Bao 2-2.
Huko Etihad hapo Jana, Tottenham
ilitinga ikiwa na Rekodi bora kwenye Ligi Kuu England ya kutoruhusu
Mabao mengi kupita yeyote lakini Jesus Navas na Sergio Aguero wa Man
City walipiga Bao 2 kila mmoja, Sandro alijifunga mwenyewe na Negredo
kufunga moja na kujikuta wakitandikwa Bao 6-0.
Bao la kwanza la Man City lilifungwa na
Jesus Navas baada Sekunde 14 tu toka Mechi iaanze na Villas-Boas
amekiri: “Ulikuwa mwanzo mgumu. Ni wazi ukifungwa Bao Sekunde 14 tu,
mipango yote inapotea pamoja na matayarisho yote uliyofanya. Kila kitu
kilikwenda ovyo kwetu kutoka Difensi bora Nchini na kuruhusu Bao 6!”
Lakini pia Tottenham sasa wamecheza
Mechi 3 za mwisho za Ligi Kuu England bila ya kufunga Bao lolote na ni
Timu za mkiani tu, Crystal Palace na Sunderland, ndizo zilizofunga Bao
chache zaidi yao.
Mechi zinazofuata kwa Tottenham ni
Alhamisi kwenye EUROPA LIGI ambapo watacheza na Tromso ya Norway na
kisha Jumapili Uwanjani kwao White Hart Lane dhidi ya Mabingwa
Manchester United kwenye Mechi ya Ligi Kuu England.
Nae Meneja wa Manchester United, David
Moyes, amesikitishwa na Difensi yake iliyoruhusu Bao la Dakika ya 90 na
kuipa Cardiff City Sare ya Bao 2-2.
Amesema: “Tulipoteza mwelekeo katika
kujihami kwani tulijipanga Mpira ukapigwa kisha Refa akasimamisha na
kurudia tena. Hilo lilimsaidia Whittingham kulenga vizuri mara ya pili
na Bo-Kyung Kim kufunga!”
Vile vile, Moyes alizungumzia tukio la
Wayne Rooney la kumpiga teke Jordon Mutch ambalo wengi walidai ni Kadi
Nyekundu ingawa Refa alimpa Kadi ya Njano tu.
Lakini Moyes amesema kulikuwa hamna nia mbaya ila ni Wachezaji wawili waliogongana baada ya Mutch kukatiza mbele ya Rooney.
Hata hivyo, Moyes pia alidokeza kitendo
cha Kiungo wa Cardiff Gary Medel anaetoka Chile kutoadhibiwa kwa kumpiga
usoni Marouane Fellaini.