Bosi wa Barcelona Luis Enrique amesema bado ana imani
wachezaji wake wataendelea kutwaa vikombe licha ya kupoteza mechi ya
Clasico dhidi ya Real Madrid
“Tayari tumesahau kabisa kufungwa kunafananaje,” Enrique alisema Jumatatu.“Timu yetu ina uwezo wa kutosha kuendelea kufanya maajabu yake kama ilivyo ada yetu.”
Licha ya kipigo cha Jumamosi, Barcelona bado inaweza kumaliza msimu na mataji matano mkononi.
Wakiwa wameshinda taji la Uefa Super Cup na Fifa Club World Cup, miamba hao wa Catalans wanaizidi Atletico Madrid pointi sita wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi ya Hispania La Liga na wametinga fainali ya Kombe la Mfalme.

“Atletico ni timu hatari sana. Itakuwa ni mechi tata sana kwetu,” alisema Enrique.
“Nina imani na wachezaji wangu na imani na Barca ambayo imekuwa ikicheza kushinda mataji kwa miaka kadhaa sasa.
“Na ndiyo sababu hatuna budi kuendelea kucheza.”
"Tunataka kutwaa vikombe vitatu"
Beki Gerard Pique anasema Barcelona hawatakaa kuombolezea kipigo cha Jumamosi kuwatoa kwenye reli ya tumaini la kushinda La Liga, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Mfalme, Mataji Matatu!
“Tunataka kuthibitisha uwezo wetu kama timu iliyofanikiwa kushinda kila kitu,” alisema beki huyo mwenye miaka 29, mchezaji wa zamani wa Manchester United.
“Tunataka kushinda Jumanne na kushinda mataji yote matatu.
“Tunakwenda kukabiliana na wapinzani wagumu ambao wanajua namna ya kukaba. Tutafanya kila kinachowezekana kutinga fainali. Hakuna mtu aliyeshawishika kama sisi.”
Kucheza dhidi ya Barca ni kama fainali kwa Atletico
Fowadi wa Argentina anayekipiga Atletico, Angel Correa ameifananisha mechi hiyo ya robo-fainali na fainali.Atletico wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa La Liga, pointi sita nyuma ya vinara wa ligi Barca, mechi saba tu zikiwa zimesalia.

“Sote tunajua jinsi Barcelona wanavyocheza,” alisema Correa.
“Tutajitahidi kucheza vizuri na tutacheza kama fainali. Tutajitahidi kutafuta matokeo mazuri ili kumalizia kazi uwanja wa nyumbani tukiwa na mashabiki wetu.”
Beki Diego Godin anatarajiwa kuanza baada ya kusumbuliwa na majeraha ya misuli.
Wapinzani wanaofahamiana vema
Hii ni mara ya 13 Barcelona na Atletico zinakutana kwa kipindi kisichozidi miaka mitatu.Barcelona wameshinda mara sita, Atletico ikishinda mara ya mwisho robo fainali ya Aprili 2014.