Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, ameshakazia umuhimu wa Mechi hii ya kwanza na kuitaka Timu yake ianze kwa ushindi ikiwa wanataka kutwaa Ubingwa.
Mechi hii ni Dabi ya kwanza ya Msimu mpya inayozikutanisha Klabu za Jijini London huku Arsenal ikiwa na Mchezaji mpya mmoja tu ambae ni Kipa Petr Cech waliemnunua kutoka Chelsea.
Kwenye Mechi zao za kabla Msimu kuanza Arsenal walionyesha ungangari wao na walihitimisha kwa ushindi dhidi ya Mabingwa wa England Chelsea Wikiendi iliyopita huko Wembley walipoitungua 1-0 na kutwaa Ngao ya Jamii.
Kwenye Mechi hii na West Ham, Arsenal huenda ikamkosa Fowadi wao kutoka Chile, Alexis Sanchez, ambae alichelewa kurudi mazoezini baada ya kupewa muda zaidi wa vakesheni baada ya kuisaidia Nchi yake kubeba Copa America Mwezi uliopita.
Pia Arsenal itamkosa Kiungo Jack Wilshere ambae amevunjika mfupa wa Enka wakati akiwa mazoezini Wiki iliyopita.

Wenger amesema: “Tupo tayari kupigana. Lengo letu ni kuanza kwa kasi. Msimu uliopita baada ya Gemu 12 tulikuwa Pointi 15 nyuma ya Chelsea lakini katika Gemu zilizobakia 26 tulichukua Pointi 58 na Chelsea 55 na hii inamaanisha tulianza vibaya. Ngoja tujaribu kuanza vizuri!”

Kwa Meneja mpya wa West Ham, Slaven Bilic, Mechi hii yake ya kwanza ya Ligi Kuu England inakuja katika Wiki mbaya baada ya Juzi Alhamisi kutupwa nje ya UEFA EUROPA LIGI walipofungwa 2-1 na Astra huko Romania katika Mechi ya Marudiano baada ya Sare 2-2 katika Mechi ya Kwanza.
Kwenye Mechi hii, West Ham itawakosa Mafowadi wake Enner Valencia na Andy Carroll ambao ni Majeruhi.
Baada ya kuishuhudia Arsenal ikicheza Emirates Cup, Bilic alisema: “Ni Arsenal ile ile na wanapenda kumiliki mpira. Ni wepesi na ukipoteza mpira ni hatari sana kwako.”
Mechi nyingine za Ligi Kuu England ambazo zitachezwa Jumapili ni kati yaNewcastle na Southampton na kisha Stoke City na Liverpool ikiwa ni marudiano ya Mechi yao ya mwisho ya Ligi Msimu uliopita ambayo Stoke waliishindilia Liverpool 6-1.