Mashabiki zaidi ya 200 wa Mbeya City FC wamesafiri salama jijini
Mwanza wakitoka jijini Mbeya tayari kuisapoti timu yao itakapoingia
Uwanjani wa CCM Kirumba keshokutwa Jumamosi kupepetana na Kagera Sugar
FC kutoka Bukoba, Kagera katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara (VPL).
Akizunguma mapema leo kiongozi wa msafara wa mashabiki hao
Timoth Mwalongo ‘Mkandalasi’, amesema kuwa wanajisikia fahari kuzunguka
maeneo mengi ya nchi hii wakiisapoti timu yao kwa sababu siku zote
imekuwa ikiwapa furaha tangu ilipoanzishwa mwaka 2011 licha matokeo
mabaya kwenye mechi nne za mwanzo wa ligi ya msimu huu.“Tumekuja Mwanza kuisapoti timu yetu hakika tutaifunika CCM Kirumba, huu ni utamaduni wetu tunajisikia fahari sana kusafili kwa ajili ya kusapoti timu yetu, hii ni timu pekee ambayo imekuwa ikitupatia furaha tangu ilipoanzishwa na sisi kuamua kuweka mioyo yetu kwake, tuko zaidi ya 200, tunaimini timu hii mpaka basi hata wikiendi tunajua itatupatia furaha.
“Mbeya City ni timu ya kizazi cha sasa kwa hiyo popote ilipo na sisi tutakuwapo kamwe hatuwezi kuiacha hata iweje” amesema Mkandalasi akinukuliwa na mtandao rasmi wa Mbeya City FC leo.
City iliyomaliza nafasi ya tatu msimu uliopita wa VPL, imekuwa na mwanzo mbaya msimu huu wa ligi hiyo baada ya kupoteza mechi nne mfululizo mwanzoni mwa msimu dhidi ya Azam FC, Mtibwa Sugar FC na Stand United FC.
