MSHAMBULIAJI
wa Azam FC ya Dar es Salaam, Gaudence Exavery Mwaikimba amesema kwamba
anamshukuru Mungu amekuwa na bahati nzuri ya kufunga mabao kwenye Uwanja
wa Sokione mjini Mbeya.
Mwaikimba
ameyasema hayo leo wakati timu yake inaondoka kwenda Mbeya, kumenyana
na wenyeji Mbeya City Council (MCC) katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara kwenye Uwanja huo.
Azam
inataka pointi tatu katika mchezo huo itangaze ubingwa na Mwaikimba
amesema; “Mbeya ni nyumbani, nimecheza sana pale Sokoine tangu nipo
mdogo sana, Uwanja ule naujua vizuri na hata kwenye giza naweza kucheza,
uzuri nina bahati ya kufunga kwenye Uwanja ule,”.
Mshambuliaji
huyo wa zamani wa Tukuyu Stars na Prisons zote za Mbeya amesema kwamba
anakubalika sana Mbeya na ana mashabiki wengi, ambao hao humuunga mkono
anapokuwa amevaa jezi ya timu yoyote.
Azam
FC inaongoza Ligi Kuu iliyofikia ukingoni kwa pointi zake 56 baada ya
kucheza mara 24, ikiwafunga tela mabingwa watetezi, Yanga SC wenye
pointi 52 za mechi 24 pia na Mbeya City pointi 46 za mechi 24 katika
mbio za ubingwa.
Iwapo,
Azam itaifunga Mbeya City itajihakikishia ubingwa, kwani itafikisha
pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote baada ya
mechi za mwisho Aprili 19.
Yanga
SC ambayo kesho inacheza na JKT Oljoro mjini Arusha, itamaliza na
mahasimu Simba SC Uwanja wa Taifa, wakati Azam itamaliza na JKT Ruvu
Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Hata
hivyo, Yanga SC wana malalamiko Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) dhidi
ya mchezaji Mohamed Netto wa JKT Mgambo aliyecheza siku wanafungwa
mabao 2-1 na timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa Uwanja wa Mkwakwani,
Tanga.
Lakini
kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu, malalamiko hayo hayawezi kupangua
matokeo iwapo madai ya Yanga yataonekana yana ukweli, bali zitatolewa
adhabu tu kwa ama kwa timu au mchezaji.www.fulu viwanja blogspot.com