NAHODHA
wa Yanga SC, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ jana ameingia kambini katika
hoteli ya Kiromo, Bagamoyo, Pwani kujiunga na wenzake kwa ajili ya
mchezo wa Jumapili dhidi ya JKT Ruvu.
Cannavaro
alikuwa anaumwa Malaria tangu arejee kutoka Tanga mapema wiki hii,
ambako mwishoni mwa wiki timu yake ilifungwa mabao 2-1 na Mgambo JKT
Uwanja wa Mkwakwani.
Mganda,
Emmanuel Okwi bado hajapatikana na viongozi wanalalamika hata simu yake
haipatikani, wakati mgonjwa mwingine wa Malaria, kiungo Haruna
Niyonzima naye bado anajiuguza nyumbani kwake.
Beki
Kevin Yondan ameondolewa katika programu ya mchezo ujao kwa kuwa
anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano na hayupo kambini na mchezaji
mwingine ambaye sababu za kutokuwepo kwake kambini hazijulikani ni
Athumani Iddi ‘Chuji’, ingawa watu wake wa karibu wanasema ana matatizo
ya kifamilia.
Habari
njema tu ni kwamba, makipa wote watatu waliosajiliwa msimu huu Yanga
SC, Juma Kaseja, Deo Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’ wapo
kambini na wanaendelea na mazoezi.
Baada
ya kupoteza pointi tatu zinazowafanya waachwe mbali na kidogo na Azam
FC katika mbio za ubingwa, Yanga SC itashuka dimbani Jumapili hii
kumenyana na timu nyingine ya Jeshi la Kujenga Taifa, JKT Ruvu Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Azam
FC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 53 baada ya kucheza mechi 23,
ikifuatiwa na Yanga SC yenye pointi 46 za mechi 22 na Mbeya City yenye
pointi 45 za mechi 23 ni ya tatu.
Wakati
Yanga SC itacheza na JKT Ruvu Jumapili Uwanja wa Taifa, Mbeya City
itacheza na Ashanti United Jumamosi Uwanja wa Azam Complex, Dar es
Salaam.
Azam
FC ilikuwa icheze na Ruvu Shooting Jumapili hii pia, Uwanja wa
Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani lakini mchezo huo umesogezwa mbele hadi
Aprili 9, kutokana na timu hiyo kuwa na wachezaji wengi katika kikosi
cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro
Heroes.
Ngorongoro
Heroes ipo Nairobi, Kenya tangu jana kwa ajili ya mechi ya kuwania
kucheza Fainali za Vijana Afrika, itakayochezwa Jumapili ya Aprili 6
mwaka huu Uwanja wa Machakos ulioko kilometa 80 kutoka jijini Nairobi na
Azam ina wachezaji zaidi ya watano kwenye kikosi hicho.
Hao ni Aishi Manula, Bryson Raphael, Gardiel Michael, Kevin Friday, Mudathir Yahya, Farid Mussa na Hamad Juma.