KLABU za Ligi Kuu England zimetumia Pauni 660 milioni kwenye
uhamisho wa wachezaji wa kimataifa kwa mwaka jana pekee, huku zaidi ya
pauni 50 milioni zikitumika kwenye ada za kulipwa mawakala, imeripoti
Fifa.
Klabu za Italia zinafuatia kwa kushika namba mbili
kwa kutumia pesa nyingi baada ya kuponda pauni 286 milioni, kisha
inakuja Ufaransa (pauni 253milioni), Hispania (pauni 192 milioni) na
Ujerumani (pauni 144 milioni).
Nchi ya Brazil imeongoza kuwa na wachezaji wengi waliouzwa ng’ambo, ambapo jumla ni wachezaji 1,558 sawa na asilimia 13.
Klabu za Hispania zimeingiza pesa nyingi zaidi
kwenye usajili huo kwa mwaka jana baada ya kuvuna pauni 150 milioni
kutokana na kuuza wachezaji wake ng’ambo.
“Kuna klabu chache sana zilizofanya usajili mkubwa
ambao ulitetemesha sokoni, lakini usajili mwingine ulikuwa wa kawaida
tu,’ alisema Mark Goddard, meneja wa masuala ya uhamisho wa wachezaji
Fifa.Kwa England usajili mkubwa wa mchezaji aliyehamia kwenye Ligi Kuu
ni ule wa Arsenal walipomnasa Mjerumani Mesut Ozil kwa pauni 42.4
milioni kutoka Real Madrid, wakati uhamisho wa kuuza nje ya nchi ni ule
wa Gareth Bale kutoka Tottenham kwenda Madrid kwa pauni 85.3 milioni.