
Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo.
MUDA mfupi baada ya kuingia mkataba wa miezi
sita na kocha, Hans Van Der Pluijm, Yanga imetoboa siri kuwa ilishindwa
kumpa kazi hiyo kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo, aliyetaka
alipwe mshahara wa Sh 28.4 Milioni kwa mwezi.
Jana Jumatatu mchana, Yanga ilisaini mkataba wa
miezi sita na Van Der Pluijm ambaye ni raia wa Uholanzi. Mara tu
aliposaini, kocha huyo aliondoka kwenda Uturuki kujiunga na kikosi
kilichopo huko kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu
Bara na mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Lakini wakati hilo likitimia, Mwenyekiti wa Kamati
ya Usajili ya Yanga, Abdallah Bin Kleb, aliliambia Mwanaspoti kuwa
kabla ya kukubaliana na Mholanzi huyo, walizungumza na Mskochi Bobby
Williamson wa Gor Mahia ya Kenya ambaye hakuonyesha nia kama alivyofanya
Mbelgiji Adel Amrouche wa Harambee Stars, ndipo wakahamia kwa Mbrazili
Maximo.
“Maximo alikubali kuja Yanga. Lakini alitaka
mshahara mkubwa, dola 18,000 (Sh28 milioni) kwa mwezi. Tukashindwa maana
hizo ni fedha nyingi kwetu, viongozi tulijadialiana sana, tukaona
hatuwezi kumlipa,” alisema Bin Kleb.
“Unajua fedha za Yanga zinatokana na Wanayanga
wenyewe, sasa tusingeweza kuingia mkataba na Maximo halafu tupate tabu
ya kumlipa.”
Zaidi ya makocha 50 walielezewa kuomba kazi ya
kuwafundisha mabingwa hao wa Tanzania Bara kabla ya klabu hiyo
kumalizana na Van Der Pluijm.
Kocha huyo anachukua nafasi ya Mholanzi mwenzake,
Ernest Brandts, ambaye alipewa notisi hivi karibuni kutokana na uongozi
kueleza kutoridhishwa na kiwango chake. Ilikuwa siku chache baada ya
timu hiyo kufungwa na Simba mabao 3-1 katika mechi ya Nani Mtani Jembe.