MENEJA WA KILIMANJARO (KATIKATI) AKIWAKABIDHI VIFAA MAKAMU MWENYEKITI WA SIMBA, MZEE KINESI NA MSEMAJI WA YANGA, BARAKA KIZUGUTO. VIFAA HIVYO NI KWA AJILI YA MECHI YA NANI MTANI JEMBE JUMAMOSI IJAYO. |
Kampuni ya
Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager imekabidhi
jezi kwa timu za Simba na Yanga kwa ajili ya mechi ya Nani Mtani Jembe
itakayochezwa Jumamosi kuanzia saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Kampeni ya
Nani Mtani Jembe iliyozinduliwa Oktoba 6 mwaka huu itamalizika Jumamosi
kwa klabu za Simba na Yanga kuchuana vikali pamoja na kuwania Sh milioni 100
zilizotengwa na Kilimanjaro Premium Lager ambao ni wadhamini wakuu wa timu
hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meneja wa Kilimanjaro Premium Lager George Kavishe alisema wanakabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh milioni 6.8 kwa ajili ya kuzipa mwonekano mpya timu hizo katika mechi hiyo.
“Bado tunaendelea kuhesabu
siku kuelekea siku ya mwisho ya kampeni yetu ya Nani Mtani Jembe Desemba 21
mwaka huu, Yanga ndio hadi sasa wanaongoza wakiwa na Sh Mil 91 na Simba wao
wana Sh Mil 9,” alisema.
Katika
kampeni hiyo ya Mtani Jembe mteja atabandua ganda la kizibo cha bia ya Kilimanjaro
Premium Lager ataona namba. Ataandika jina la timu yake (SIMBA au YANGA)
ikifuatiwa na namba hiyo ya kwenye kizibo kasha atatuma kwenda namba 15440 na
kuipa nafasi timu yake.
Kwa upande wake Makamu
Mwenyekiti wa Simba Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ aliwashukuru wadhamini hao
Bia ya Kilimanjaro kwa vifaa hivyo huku akitamba timu yake kuibuka na ushindi.
Naye Ofisa
Habari wa Yanga Baraka Kizuguto aliwashukuru wadhamini hao kwa kuwafanyia mambo
mazuri na kuahidi kuendeleza mambo mazuri kwao na wataibuka na ushindi katika
mechi hiyo.