ROBERT
LEWANDOWSKI, Straika hatari kutoka Poland anaechezea Borussia Dortmund
huko Germany, atatangaza rasmi Klabu ipi atahamia hapo Januari 2.
Hilo ni kwa mujibu wa Mtangazaji wa
Kituo kimoja cha TV huko Poland, Mateusz Borek, ambae alitoboa habari
hizi kwenye Mtandao wa Twitter mara tu baada ya Lewandowski kurushwa
kwenye Kipindi cha Mtangazaji huyo, 'Football Café', na kufanya habari
hizo ziwe za kuaminika.
Mkataba wa sasa wa Lewandowski na
Borussia Dortmund unamalizika mwishoni mwa Msimu na hilo linamfanya Staa
huyo awe huru kuanzia Januari 1, kwa mujibu wa FIFA, kufikia
makubaliano ya awali, kabla kusaini Mkataba wa Kudumu, na Klabu yeyote
nyingine inayomtaka kumnunua.
Inaaminika Mchezaji huyo atahamia kwa
Mabingwa wa Bundesliga, Ulaya na Dunia, Bayern Munich, ingawa mwenyewe
hajathibitisha hilo hadi sasa na hivyo kuacha mlango wazi kwa kila uvumi
kuzagaa.
Klabu kadhaa Vigogo Barani Ulaya
zimekuwa zikimwinda Straika huyo hatari kwa Magoli na Siku za nyuma
amekuwa akihusishwa sana na kuhamia Manchester United, Barcelona na Real
Madrid.