KIUNGO wa zamani Mpiganaji na Mahiri wa
Italy na AC Milan Gennaro Gattuso amekanusha vikali tuhuma za kuhusika
na upangaji matokeo Mechi kiasi cha kudai kuwa endapo atapatikana na
hatia atajiua.
Gattuso, ambae Mwaka wa 2006 alitwaa
Kombe la Dunia akiwa na Italy, mapema Jumanne alitajwa na Vyombo vya
Habari vya Italy kuwa anahusika kwenye tuhuma za upangaji matokeo Mechi
na yupo kwenye uchunguzi unaoendeshwa na Mwendesha Mashitaka wa Ofisi ya
huko Cremona.
Pamoja na Gattuso pia yupo Kiungo wa
zamani wa Lazio Cristian Brocchi na wote wanahusishwa na tuhuma kuwa
walikula njama katika Msimu wa 2010/11 kupanga Matokeo ya Mechi za Serie
A na nyinginezo.
Inadaiwa Gatusso na Brocchi walikuwa na
uhusiano kwa Simu na Watu wanne ambao wamekamatwa na Polisi kwa madai
hayo ya kupanga Matokeo Mechi.
Mara baada ya kuibuka tuhuma hizo,
Gattuso alikaririwa kwenye Sky Sport Italia akisema: “Sijawahi hata Siku
moja kuwa na fikra ya kupanga Matokeo Mechi. Kama watathibitisha niko
tayari kwenda Mtaani, na najua hiki ni kitu kizito kusema, nitajiua
mwenyewe.”
Aliongeza: “Yeyote anaenijua mimi anajua
sikubali kufungwa hata Mazoezini, na hata kwenye Mchezo wa Karata na
Rafiki zangu. Nimekasirika na nimedhalilishwa. Nataka kujisafisha nisiwe
na doa kwenye maisha yangu ya Soka. Sijacheza Kamari maishani mwangu!”
Gattuso, mwenye Miaka 35, alistaafu
kucheza Soka mapema Mwaka huu na kuingia kwenye Ukocha lakini amekuwa
hana kazi tangu atimuliwe kuifundisha Palermo, inayocheza Serie B, Mwezi
Septemba.
Brocchi ni Kocha wa Timu ya Vijana ya AC Milan.