NAHODHA wa England Steven Gerrard pamoja
na Beki Kyle Walker wataikosa Mechi ya Nchi yao na Chile hapo Ijumaa
baada ya kupata maumivu kidogo lakini wanatarajiwa kucheza Mechi ya
Jumanne dhidi ya Germany.
Wakati Gerrard bado anajiuguza tatizo la
Paja aliloumia wakati Klabu yake Liverpool inaifunga Fulham Wikiendi
iliyopita, Kyle Walker alikosa Mazoezi ya England hapo Jumatano akiwa na
tatizo la Mguu na hii inafuatia kujitoa kwenye Kikosi Wachezaji wawili
wa Manchester United, Michael Carrick na Danny Welbeck, ambao wameumia.
Mbali ya Majeruhi hao, Kambi ya England
pia ilivurugika mwanzoni tu baada ya kulazimika kubadilisha Kituo chao
cha kawaida toka National Football Centre kwenda Watford kukimbia
kuambukizwa Ugonjwa wa Tumbo uliozuka kwenye Kituo hicho chao cha
kawaida.
Wakati huo huo, Fowadi wa Chile
anaechezea Klabu ya Barcelona, Alexis Sanchez, amewasha moto wa Mechi
kati ya England na Chile pale alipotamka Wachezaji wa England wako
‘laini’ kutokana na Maisha yao ya kudekezwa na hilo limepokewa vibaya
toka Kambi ya England.
Straika wa Southampton, Rickie Lambert,
amesema sasa hawahitaji tena motisha toka kwa Meneja wao kwani kauli
hiyo ya Sanchez imewakera.
Lambert ametamka: “Kwa kauli ile huhitaji motisha tena!”