
HATUA za Makundi za Mashindano ya Klabu Barani Afrikaza CHAMPIONZ LIGI, CL, na za Kombe la Shirikisho, CC, zitapanuliwa kutoka Klabu 8 za sasa hadi 16 Mwakani 2017.
Rais wa CAF Issa Hayatou ametangaza hilo huko Mexico City Nchini Mexico alipokutana na Maafisa wa Vyama vya Soka vya Afrika walioko huko kwa ajili ya Kongresi ya FIFA.
Rais huyo amesema Mfumo wa Makundi wa Mashindano hayo mawili ya Klabu Barani Afrika utakuwa ni wa Ligi ndogo wa Makundi Manne ya Timu 4 kila moja.
Awali, tangu 1997, kulikuwa na Makundi Mawili ya Timu 4 kila moja na Washindi wa kila Kundi kutinga Fainali lakini kuanzia 2001 kukaanzishwa Nusu Fainali ambapo Washindi na Washindi wa Pili wa kila Kundi walishiriki.
CC nalo lilikuwa na Mfumo kama CL.
Rais Hayatou pia alithibitisha Zawadi za Fedha kwa Mashindano hayo zitaongezeka baada ya CAF kusaini Dili mpya ya Matangazo na Masoko ya Miaka 12 yenye thamani ya zaidi ya Dola Bilioni 1.
Kwa sasa Bingwa wa CL huzoa kitita cha Dola Milioni 1.5 na yule wa CC hupata Dola 660,000.