MABINGWA WATETEZI na Vinara wa La Liga FC Barcelona Usiku huu wamenasa huko Estadio Mestalla walipotoka Sare ya 1-1 na Valencia iliyoshuhudiwa na Meneja wao mpya Gary Neville aliekuwa Jukwaani.
Barca walitangulia kufunga kwa Bao la Luis Suarez la Dakika ya 58 lakini Dogo wa Miaka 19 wa Valencia Santiago Mina alisawazisha katika Dakika ya 86 na kuufanya Uwanja wote wa Mestalla uinuke kwa furaha.
Gary Neville, alieteuliwa kuwa Kocha Mkuu mpya wa Valencia hadi mwishoni mwa Msimu huu, Leo alikuwa Jukwaani kuishuhudia Timu yake na ataanza kazi yake rasmi Wiki ijayo.
Mapema hii Leo, Real Madrid iliichapa Getafe Bao 4-1 kwa Bao za Kipindi cha Kwanza za Karim Benzema, Bao 2, Gareth Bale na Cristiano Ronaldo huku Bao la Getafe likifungwa Dakika ya 70 na Alexis Ruano Delgado.
Atletico Madrid waliifunga Granada 2-0 kwa Bao za Diego Godin na Antoine Griezmann na kubaki Nafasi ya Pili wakiwa Pointi 2 nyuma ya Barcelona na Pointi 2 mbele ya Timu ya 3 Real.
Valencia wapo Nafasi ya 7.