KIPA
MPYA wa Manchester United, Victor Valdes, ambae ni Nguli wa Barcelona
na Timu ya Taifa ya Spain, anatarajiwa kuichezea kwa mara ya kwanza
kabisa Klabu yake mpya hapo Ijumaa Usiku kwenye Mechi ya Ugenini ya
Raundi ya 4 ya FA CUP dhidi ya Cambridge United.
Valdes, mwenye Miaka 32 ambae ni Mchezaji wa Kimataifa wa Spain,
amesaini kuichezea Manchester United kwa Mkataba wa Miezi 18 Wiki
iliyopita na amekuwa akifanya Mazoezi na Timu hiyo kwa Miezi miwili sasa
katika harakati zake za kurudia hali yake ya kawaida baada ya kuumia
vibaya Goti lake Mwezi Machi.
Akiwa na Barcelona, Valdes alitwaa Ubingwa wa La Liga mara 6 na UEFA
CHAMPIONZ LIGI mara 3 na kabla Msimu uliopita kumalizika alitangaza
kuondoka Barca baada ya mwenyewe kukataa kuongeza Mkataba wake.
Cambridge United, ambayo inacheza Ligi 2, ndio Timu pekee ya Daraja
la chini kabisa iliyobakia kwenye Raundi ya 4 ya FA CUP na Mechi hii
itakayochezwa Uwanjani kwao Abbey Stadium huko Cambridge ni ya
Kihistoria kwao ingawa waliwahi kufika Robo Fainali ya FA CUP mara mbili
katika Miaka ya 1990 na 1991.
Kwenye Msimamo wa Ligi 2, Cambridge United wako Nafasi ya 12.