Social Icons

Pages

Wednesday, 15 January 2014

YANGA YAMLUNDIKIA VYEO VITATU BABU MHOLANZI, MKURUGENZI YEYE, KOCHA YEYE NA MENEJA PIA…HAIJAWAHI KUTOKEA


YANGA  ya Dar es Salaam imempa vyeo vitatu mtaalamu wa soka kutoka Uholanzi, Johannes Franciscus 'Hans' van der Pluijm, ambavyo ni Ukurugenzi wa Ufundi, Kocha Mkuu na Meneja wa timu ya soka, ambayo mwezi ujao itashiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Hata hivyo licha ya kupewa vyeo vitatu kocha huyo ambaye amerithi mikoba ya mholanzi mwenzake, Ernie Brandts, amesaini mkataba wa kuitumikia Yanga kwa muda wa miezi sita.
Akizungumza leo katika makao makuu ya klabu hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, alisema kuwa wameamua kumpa vyeo hivyo vitatu ili aweze kuyatumikia vyema majukumu yake na kubwa ni klabu hiyo ifanye vizuri katika mashindano ya kimataifa na kutetea ubingwa wao.
Sanga alisema pia wamempa mkataba mfupi kocha huyo kwa sababu wanataka kwanza waone 'matunda' na kazi yake na kutakuwa na kamati maalumu itakayofuatilia utendaji wake wa kazi.
Makamu huyo alitaja moja ya majukumu ya Pluijm ni kuwasilisha taarifa ya maandishi ya maendeleo ya timu kila wiki huku akitakiwa kuwafanya wachezaji wawe na nidhamu ndani na nje ya mchezo.
"Tunataka kocha awe kama mzazi au mlezi, kuna mambo tuliyagundua kwa Brandts lakini sasa hatutaki yarejee, tunataka kwenda hatua nyingine ya kisasa kwenye uongozi na timu," Sanga aliongeza.
Alisema kwamba Yanga imejipanga kuhakikisha inatetea ubingwa na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa mwaka huu.
Alieleza kuwa viongozi na wachezaji wamedhamiria kurejesha heshima ya timu yao ndani na nje ya nchi msimu huu.
Mwaka huu Yanga pia itaiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) ambayo yatafanyika mwezi Juni jijini Kigali nchini Rwanda.
Wakati huo huo: Uongozi wa Yanga umewataka wanachama wa klabu hiyo kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini kujitokeza kwa wingi katika mkutano mkuu wa mwaka utakaofanyika Jumapili Januari 19 kwenye ukumbi wa PTA (Sabasaba), jijini Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, amesema leo kwamba mkutano huo utafanyika kuanzia saa 3:00 asubuhi na ndiyo sehemu muhimu kwa wanachama kufikisha mawazo yao ya kujenga timu na klabu hiyo.

Sanga alisema kuwa katika mkutano huo watajadili mambo muhimu ya klabu ikiwemo mikakati ya kutetea ubingwa na kujiandaa na mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
 
FULU VIWANJA