Social Icons

Pages

Sunday, 5 January 2014

SIMBA SC YAFUZU ROBO FAINALI MAPINDUZI…AMRI KIEMBA SHUJAA

SIMBA SC imefanikiwa kufuzu Robo Fainali ya Kombe la Mapinduzi, kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMKM usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Kwa matokeo hayo, Simba SC inamaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi B, ikiwa na pointi saba, mabao mawili ya kufunga na haijafungwa, nyuma ya KCC ya Uganda yenye pointi saba pia, mabao sita ya kufunga na mawili ya kufungwa.
Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa bao hilo moja lilifungwa na Amri Ramadhani Kiemba kwa kichwa, akiunganisha krosi maridadi ya Ali Badru Ali dakika ya tano.
Kocha Mcroatia Zdravko Logarusic akiiongoza timu kwa mara ya kwanza kwenye mashindano haya tangu arejee kutoka mapumzikoni, alifanya mabadiliko makubwa katika kikosi cha kwanza leo, akiwapanga wachezaji wengi wa benchi.
Hata hivyo, wachezaji hao hawakumuangusha kwa kucheza vizuri na kama wangekuwa makini zaidi wangeweza kuondoka na mabao zaidi kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili, KMKM inayofundishwa na Ali Bushiri ilicharuka na kukaribia kufunga mara kadhaa, lakini hata hivyo bahati haikuwa yao na hadi kipyenga cha kuhitimisha mchezo kinapulizwa, walilala 1-0.
KMKM sasa inasubiri mustakabali wake wa kusonga mbele katika nafasi mbili maalum kwa makundi yote, kuungana na timu sita zitakazofozu moja kwa moja kutoka makundi hayo. 
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Yaw Berko, William Lucian ‘Gallas’, Omar Salum/Miraj Athumani, Gilbert Kaze, Donald Mosoti/Joseph Owino, Abdulhalim Humud, Uhuru Suleiman/Said Ndemla, Amri Kiemba, Betram Mombeki/Zahor Pazi, Ali Badru na Edward Chistopher/Adeyoum Saleh.
KMKM; Mudathir Khamis, Pandu Hajji, Haidhurun Juma, Khamis Ali, Iddi Kambi, Ibrahim Hatibu, Nassor Omar/Hajji Simba, Maulid Kapenta, Vincent Kamanya na Machano Abdallah. 
 
FULU VIWANJA