BOSI
wa Liverpool Brendan Rodgers amesisitiza Timu yake bado ipo kwenye
kinyang’anyiro cha Ubingwa licha ya vipigo viwili mfululizo
vilivyoing’’oa kileleni na kuitupa Nafasi ya 5.
Liverpool walikuwa kileleni Siku ya
Krismasi lakini sasa wapo Nafasi ya 5 Pointi 6 nyuma ya Vinara Arsenal
baada kutandikwa na Manchester City na Chelsea.
Hata hivyo Brendan Rodgers bado ana
matumaini na amesema: “Hamna sababu kwa nini tusigombee Ubingwa. Kitu
muhimu kwetu ni kuwa bado tupo kwenye kinyang’anyiro!”
Jana Usiku Liverpool walipigwa Bao 2-1
Uwanjani Stamford Bridge na Chelsea na hii imefuatia kipigo kingine cha
2-1 Boksing Dei huko Etihad walipofungwa na Man City.
Lakini kipigo toka kwa Chelsea, ambao
wako Pointi 4 mbele ya Liverpool, kimeathiri sana Kikosi cha Brendan
Rodgers baada Wachezaji kadhaa kuumia kwenye Mechi hiyo.
Beki Mamadou Sakho aliumia Musuli za Pajani, Joe Allen na Jordan Henderson nao pia walipata maumivu.
Rodgers amekiri Kikosi chake ni kidogo
na kina uhaba wa Wachezaji lakini wanatarajia kuimarika Mwezi Januari
kwa kununua Wachezaji Dirisha la Uhamisho likifunguliwa na pia kupona
kwa Nahodha wao Steven Gerrard na Straika Daniel Sturridge ambao wote
walikuwa wameumia na kuzikosa Mechi kadhaa kutaongeza nguvu.
Katika Raundi ya Pili ya Ligi Kuu
England inayoanza Januari Mosi, ukiwaondoa Manchester United, Timu zote
za juu 8 itabidi ziende Anfield kurudiana na Liverpool na hilo limempa
faraja Rodgers ambae ametamka: “Ikifika Januari tunategemea Wachezaji
wote watakuwa fiti na tutaongeza nguvu Kikosini na Raundi ya Pili
tutakuwa vyema. Tukibahatika kukosa majeruhi kipindi hicho, ni wazi
tutapigania Ubingwa!”