TIKETI karibu 230,000 zilizotangazwa kuuzwa katika Awamu ya Pili ya Mauzo ya Tiketi za Fainali za Kombe la Dunia za huko Brazil Mwaka 2014 ziliuzwa ndani ya Masaa 7 tu tangu mauzo yake yaanze kwenye TOVUTI ya FIFA hapo Jana.
FIFA imesema mauzo hayo yalichangamka kupita yale Mauzo ya Awamu ya Kwanza ambapo Tiketi 890,000 ziliuzwa.
Maombi zaidi ya Milioni 6.2 ya kununua Tiketi yamepokewa ambayo ni mara mbili ya Tiketi ambazo zipo.
Katika Mauzo ya Awamu ya Kwanza, Tiketi Milioni 1.1 ziliwekwa Sokoni.
Safari hii, Mauzo ya Tiketi hayakuhusu
zile Mechi zenye mvuto mkubwa ambazo ni pamoja na Mechi ya Ufunguzi wa
Fainali hizo hapo Juni 12 huko Mjini Sao Paulo, Brazil, Fainali ya Julai
13 Uwanja wa Maracana Mjini Rio de Janeiro, Nusu Fainali mbili na Mechi
zote za Makundi za Wenyeji Brazil.
Tiketi zaidi za Fainali hizo zitauzwa Desemba 8 mara baada ya Droo ya kuamua wapi na lini Timu 32 za Fainali hizo zitacheza.
FIFA imesema Asilimia 8 ya Tiketi zitakuwepo kwa ajili ya Mashabiki wa Nchi ambazo zitacheza Raundi ya Kwanza ya Fainali hizo.
FIFA imesema kulikuwa na msongamano
kwenye Tovuti yao wakati wa Mauzo ya Tiketi kukiwa na Watu Milioni 3.6
wakitembelea Tovuti hiyo na ilichukua wastani wa Dakika 45 kwa Watu
kuifikia Kurasa ya Tovuti ya Mauzo.
Kila Muombaji kununua Tiketi anaruhusiwa kununua Jumla ya Tiketi 4 na si zaidi ya Mechi 7 kati ya Mechi zote 64.